Waziri wa madini Angela Kairuki |
“Wakati tunasubiri taratibu za serikali kukamilika kabla ya kuanza majadiliano, tunapenda kumhakikishia Mheshimiwa Rais John Magufuli na Watanzania kwa ujumla kwamba sisi kama TanzaniteOne tutatoa ushirikiano utakaowezesha kuwa na hitimisho lenye tija kwa taifa letu,” ilisema taarifa kutoka kwenye uongozi wa kampuni hiyo.
Taarifa hiyo rasmi kutoka Bodi ya Uongozi wa TanzaniteOne Limited iliyosainiwa na Katibu wa Kampuni, Kisaka Mnzava, inasema kuwa viongozi wake wako tayari kufuata maelekezo yoyote yatakayotolewa na serikali baada ya mazungumzo yanayotarajiwa kufanyika baina ya kampuni hiyo na serikali.
“TanzaniteOne iko tayari kuingia kwenye majadiliano na serikali kwa ajili ya kufanya mapitio ya mkataba husika pamoja na kurekebisha taratibu zote za uchimbaji na biashara ya madini nchini kwa manufaa ya Watanzania wote,” alifafanua Mnzava.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo rasmi, TanzaniteOne itashirikiana bega kwa bega na timu ya serikali itakayoundwa kwa ajili ya kutekeleza wajibu huo, lengo likiwa ni kuwezesha madini ya tanzanite yanayopatikana Tanzania peke yake, kuwa yenye manufaa kwa taifa.
“Tunafanya hivyo kwa sababu mbili: Kwanza ni kutambua juhudi zinazofanywa na Rais John Magufuli na hatua anazochukua kulinda rasilimali za taifa na kuhakikisha kuwa madini yanawanufaisha Watanzania wote kwa ujumla.”
“Pili tunaamini kuwa wabia wa kampuni ya TanzaniteOne, mbao ni Watanzania wazawa wana wajibu wa kushiriki katika mchakato mzima wa kuliwezesha taifa kunufaika na rasilimali za madini nchini,” waliongeza viongozi wa TanzaniteOne katika taarifa yao kutoka Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara.TanzaniteOne Mining Limited ni kampuni ya ubia baina ya wafanyabiashara wa jijini Arusha, Hussein Gonga na Faisal Shahbhat kupitia Sky Associate wanaomiliki asilimia 50 za hisa na serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (Stamico) lenye hisa 50 pia.
Wakati wa ziara yake ya uzinduzi wa Barabara ya KIA-Mirerani, Septemba 27, mwaka huu, Rais Magufuli aliagiza kupitiwa upya mkataba wa uchimbaji na biashara ya madini hayo ya vito baina ya Sky Associate na Stamico.
Oktoba 19, mwaka huu, baada ya kushuhudia kutiwa saini makubaliano baada ya mazungumzo baina ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Barrick Gold Corporation, Rais Magufuli alimuagiza Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi kwamba timu ya serikali ianze kufanyia kazi madini ya tanzanite na almasi.
Post a Comment
karibu kwa maoni