0
Matumizi ya vilevi mbalimbali ni moja ya vichocheo vinavyosababisha ongezeko la wagonjwa wa akili, huku mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mwanza ikiwa ndio vinara vya wagonjwa hao.
Mratibu wa Taifa magonjwa  ya akili na dawa za kulevya kutoka Wizara ya Afya, Shadrack Buswelu amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Morogoro leo Ijumaa.
Biswalu amesema magonjwa ya akili au afya ya akili bado yamekuwa ni tatizo kubwa katika jamii, hivyo ni mzigo kwa Taifa na duniani kwa ujumla jambo linalosababisha kurudisha nyuma maendeleo katika nyanja mbalimbali.
Amesema huduma ya afya ya akili kwa sasa inatakiwa kupewa kipaumbele mahala pa kazi, waajiri wanapaswa kuhakikisha wanawahudumia wafanyakazi wao pindi wanapoona kuna tatizo linajitokeza kwenye maeneo ya kazi.
“Mikoa ya Lindi na Mtwara inaonyesha kuwa ya mwisho kwa kuwa na wagonjwa wa akili na hii sio sababu kwamba hawapo bali idadi katika mikoa inayoongoza wamekuwa wakiripotiwa na mikoa hiyo ya mwisho ripoti yake imekuwa ni ndogo,”amesema.
Mratibu huyo ambaye hakutaka kutanja tawimu kwa namba amesema uelewa wa wananchi bado umekuwa mdogo kutokana na asilimia kubwa kukimbilia kwa waganga wa jadi badala ya kufika katika vituo vya kutolea huduma.
Amesema kwa mujibu wa taarifa ya afya akili na dawa za kulevya zinazopatikana kwenye vituo vya kutolea huduma za mwaka 2015/2016 wagonjwa 6,072 walilipotiwa, huku 2016/2017 wagonjwa waliouzuria kupatiwa matibabu ni 7,084 hivyo takwimu hizo zimekuwa zikiongezeka kila mwaka.
Alitaja baadhi ya vichocheo vya ugonjwa huo kuwa ni pamoja na unywaji pombe, matumizi ya dawa za kulevya, ugumu wa maisha unaochangiwa na msongo wa mawazo, balaa la njaa, ubakaji, mafuriko, mtu kupoteza kazi, kufukuzwa shule, vita na wamama wajawazito kutumia vilevi husababisha mtoto kuzaliwa na ugonjwa huo.
Vile vile amesema Serikali ilitoa sheria ya afya ya akili ya Mwaka 2008 ambayo imekuwa ikitoa maelekezo ya namna gani huduma zitakavyotolewa nchini,akasisitiza kauli ya wanajamii kumuita mtu kichaa ni kosa kisheria.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top