0
Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa amemtumia ‘salamu’ Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwamba gharama za kuandaa Katiba Mpya si kubwa ukilinganisha na mahitaji ya Watanzania.

Akihutubia mamia ya watu katika viwanja vya Soko Kuu la Kwa Mromboo jijini Arusha juzi, Lowassa alimsihi Rais John Magufuli kuruhusu mjadala wa Katiba Mpya kwa kuwa ndiyo kiu ya Watanzania kwa sasa.

“Wananchi wamesema Rais Magufuli aruhusu mjadala wa Katiba Mpya, lakini waziri mkuu wake amesema ni gharama sana mimi nasema gharama hizo ukilinganisha na idadi ya watu wanaohitaji jambo hili ni kubwa sana atukubalie tujadili Katiba Mpya,” alisema Lowassa huku akishangiliwa.

Baadhi ya wabunge waliohudhuria mkutano huo ni Godblesss Lema (Arusha Mjini), Joshua Nassari (Arumeru Mashariki) na meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro.

Lowassa, awali aliwauliza wananchi: “Tunahitaji Katiba Mpya hatuhitaji?” na wananchi walijibu: “Tunahitaji.”

“Mimi pendekezo langu ni kwamba mheshimiwa Rais kwa heshima zote akubali mjadala wa Katiba Mpya,” alisisitiza Lowassa.

Hata hivyo, Lowassa aliwaambia watu waliohudhuria mkutano huo kuwa jambo jingine lililomfikisha mbele yao ni kuwashukuru kwa dhati baadhi ya Watanzania walivyompigia kura mwaka 2015, kwa sababu alizuiwa kuzunguka nchi nzima.

Awali, mgombea udiwani wa Chadema, Simon Mollel alitaja vipambele vyake kuwa ni kushughulikia kero za jamii hususan maji na kuwaomba wananchi wamchague.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top