Dodoma, Novemba 14, 2017: Serikali
imesema mapato yatokanayo na kodi ya majengo yanayokusanywa na Serikali
yameongezeka baada ya jukumu hilo kukabidhiwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA), ikilinganishwa na ilivyokuwa chini ya Halmashauri.
Hayo yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), alipokuwa
akijibu swali la msingi la Mbunge wa Bukoba Mhe. Wilfred Lwakatare (CHADEMA),
aliyetaka kujua Serikali inazipa Halmashauri ushauri gani wa kitaalam wa hatua
za kuchukua ili kuziba pengo la kibajeti.
Katika swali hilo Mhe. Lwakatare aliuliza
kuwa Serikali haioni kuwa uamuzi wa kuipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
kukusanya kodi hiyo ya majengo ni kuzidi kuipa mzigo mkubwa ambao hawatauweza.
Dkt. Kijaji alisema kuwa baada ya makusanyo
yatokanayo na kodi za majengo kuanza kukusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania
TRA katika Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji 30, yalipanda hadi kufikia
Sh. bilioni 34.09 mwaka wa fedha 2016/2017 ikilinganishwa na Sh. bilioni 28.28
zilizokuwa zimekusanywa na Serikali za Mitaa mwaka wa fedha 2015/2016.
“Makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la
asilimia 20.6 ya makusanyo halisi yaliyopatikana kutoka Halmashauri husika
kabla ya kodi hiyo kuhamishiwa TRA hali inayodhihirisha kuwa, TRA imefanya kazi
nzuri katika kukusanya mapato ikilinganishwa na kiasi kilichokusanywa na
Halmashauri hizo 30 katika mwaka wa fedha 2015/16.”. alisema Dkt. Kijaji.
“Katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha
2017/18 Julai hadi Septemba, TRA, ilipangiwa kukusanya kodi ya majengo ya kiasi
cha Sh. Bil 11.9 na kufanikiwa kukusanya kiasi cha Sh. Bil. 13.2 ikiwa ni
ufanisi wa asilimia 111”. Aliongeza Dkt.
Kijaji.
“Hatua
ya Serikali ya kukasimu jukumu la ukusanyaji wa kodi za majengo kwa TRA, haikulenga
kuzinyang’anya Halmashauri vyanzo vya mapato bali ni kuimarisha ukusanyaji
wake”. alisema Dkt. Kijaji.
Aliongeza kuwa dhamira ya Serikali ni
kuhakikisha kunakuwepo ufanisi katika ukusanyaji na matumizi ya kodi zote
zinazokusanywa ndani ya Serikali na kwamba Halmashauri zote zinapata mgao wa
fedha kwa kuzingatia makisio ya bajeti zao na makusanyo ya mapato yote ya
Serikali.
Aidha, Dkt. Kijaji alisema kuwa
Serikali inatambua kuwa kodi ya majengo imekuwa ikichangia kwa sehemu kubwa mapato
ya Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji katika kutekeleza mipango na utoaji
wa huduma na maendeleo kwa wananchi.
Katika swali la nyongeza Mhe. Lwakatare
alihoji kwa nini Serikali isichukue maoni yake ya baadhi ya majengo makubwa
yatozwe kodi na TRA na yale madogo yatozwe kodi na Halmashauri kwa kuwa
kumekuwa na changamoto kwa TRA katika ukusanyaji wa kodi hiyo na kuwatumia
Maafisa Watendaji wa Kata katika kukusanya kodi hizo ambao wameajiriwa na
Halmashauri.
Akijibu swali la nyongeza Dkt. Kijaji
amesema kuwa Serikali na Bunge lilipitisha sheria ya fedha kwamba kodi ya
majengo ikusanywe na TRA kwa lengo la kuimarisha ufanisi wake katika ukusanyaji
na matumizi.
“Serikali itaendelea kusimamia sheria
hiyo na kuhakikisha lengo la kuchukua kodi hiyo linafanikiwa na wananchi
wanapata huduma stahiki”. aliongeza Dkt. Kijaji.
Imetolewa na:
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
Post a Comment
karibu kwa maoni