0
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro
SERIKALI imewaadhibu kwa kuwachukulia hatua za kinidhamu na kisheria, watumishi 1,595 kutoka Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini baada ya kubainika ndiyo walisababisha kuajiri na kuajiriwa kwa watumishi hewa nchini.
Aidha, Serikali imesema itaendelea kubuni na kutekeleza mikakati kuhakikisha utumishi wa umma unakuwa na watumishi sahihi, wenye elimu na taaluma sahihi na wanafanya kazi mahali sahihi kuongeza ufanisi na kuiwezesha Serikali kufikia azma yake ya kuwa na uchumi wa kati na wa viwanda nchini.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro amesema hayo alipowasilisha taarifa ya uhakiki wa watumishi na vyeti vya kufaulu mtihani wa kidato cha nne, cha sita na ualimu kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali Dodoma. Hata hivyo, Dk Ndumbaro aliyetoa taarifa hiyo mwisho mwa wiki hakusema watumishi walichukuliwa hatua gani za kinidhamu kwa ushiriki wao katika suala la kuajiri watumishi hewa zaidi ya 16,000.
Alisema ili kukabiliana na tatizo la watumishi wa umma kughushi vyeti vya elimu na taaluma, Serikali na wadau wengine inabuni na kutekeleza mikakati na hatua kubaini na kudhibiti vyeti vya kughushi nchini.
Alisema ili kudhibiti watumishi kujipatia ajira kwa vyeti vya kughushi, Serikali imejipanga kuhakikisha vyeti vya taaluma na elimu vya watumishi wapya na wanaorudi katika ajira kwa sababu mbalimbali za kutoka likizo bila malipo, mikataba, uhamisho na ushikizwaji vinahakikiwa na mamlaka husika kabla ya kuingizwa na kuidhinishwa kwenye orodha ya malipo ya mishahara kuendelea na kazi walizokuwa nazo.
“Waajiri wote katika sekta ya umma wameelekezwa kutekeleza agizo hili pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria watu wote watakaobainika kuwa na vyeti vya kughushi,” alieleza Dk Ndumbaro.
Ili kuwa na taarifa sahihi za watumishi nchini, alisema Serikali imepanga kuunganisha na kuoanisha mifumo ya kimkakati ikiwemo ya taarifa za watu (Mfumo wa HCMIS, NIDA, RITA, NECTA na TRA) kuongeza usahihi wa taarifa za watumishi, kudhibiti watumishi hewa, udanganyifu wa taarifa mbalimbali za mtumishi na kurahisisha ubadilishanaji na uhakiki wa taarifa na nyaraka za watumishi wa umma.
Dk Ndumbaro alisema kwa kuanzia, uoanishaji wa taarifa za usajili za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na zilizomo kwenye Mfumo wa HCMIS unaendelea. Ndumbaro alisema Serikali ina mpango wa kupanua wigo wa uhakiki wa vyeti kwa kuhakiki vyeti vya elimu ya juu na taaluma kulingana na matakwa ya miundo ya maendeleo ya utumishi ya kila kada kwa watumishi wasio wa kada za kisiasa.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top