Anaandika Benny Mwaipaja, kutoka Dodoma.
Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Charles Kichere, akijibu baadhi ya hoja zilizowasilishwa na Sekta Binafsi wakati wa mkutano kati ya Serikali na Sekta hiyo, uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mjini Dodoma. |
WAZIRI wa Fedha na Mipango Dkt.
Philip Mpango amewaahidi wafanyabiashara na wawekezaji nchini kwamba serikali
italifanyiakazi suala la kodi katika Bajeti ijayo ya mwaka 2018/2019 ili
kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji na biashara kupitia sekta binafsi.
Dokta Mpango ameyasema hayo mjini
Dodoma katika mkutano wa tatu kati ya Serikali na Sekta binafsi ambapo masuala
mbalimbali yanayohusu kodi yamejadiliwa ikiwa ni mwendelezo wa Serikali kutaka
kuiimarisha Sekta hiyo ili iweze kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Alisema kuwa Serikali imedhamiria
kupunguza ama kuondoa kabisa kero zinazoikabili sekta binafsi ikiwemo
malalamiko ya muda mrefu ya utitiri wa kodi ili sekta hiyo iweze kuwa na nguvu
na kushiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa viwanda utakaokuza pato la
taifa na ajira nchini.
Alisema Serikali inatambua kwamba
sekta binafsi ndiyo nguzo ya ukuaji wa uchumi wa Taifa ndio maana inajitahidi
kupata maoni ya wadau kuhusu namna ya kuboresha mazingira yao ya ufanyaji
biashara na uwekezaji nchini ili kuharakisha maendeleo ya nchi.
“Ni lazima dukuduku za sekta binafsi
tuzisikilize, tuzitafakari na kuzifanyia kazi ili uchumi uweze kwenda kwa kasi zaidi
tuwaondoe wananchi wetu kwenye umasikini na vijana wetu wapate kazi’ Alisema
Dkt. Mpango.
Alisema wakati wa kuandaa bajeti yam
waka 2018/2019, serikali itaweka mfumo wa kodi utaoiwezesha Sekta Binafsi kukua
na kuimarika zaidi ili iweze kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi na kuboresha
maisha ya watanzania kwa ujumla.
“Katika mjadala huu nimefurahia kusikia maoni ya sekta binafsi
ambapo pamoja na kupendekeza maeneo ya kupunguza kodi, lakini pia wamezungumzia
namna ya kuongeza wigo wa kuongeza mapato ya Serikali” Aliongeza Dkt. Mpango.
Hata hivyo, Dkt. Mpango,
alitahadharisha jumuiya ya wawekezaji na wafanyabiashara nchini kwamba
wanapojadili juu ya masuala ya kodi, wakumbuke kwamba Serikali ina mzigo mkubwa
wa kuhudumia jamii katika masuala mbalimbali ikiwemo elimu, maji, afya,
barabara, miundombinu ya usafiri na usafirishaji ikiwemo reli na mingine mingi.
Alitolea mfano uzalishaji wa maji katika miji mikuu ya Wilaya na
miji midogo ni lita milioni 99.5 kwa siku wakati mahitaji ni lita milioni 273
kwa siku, sawa na 36.4%.
“Miradi ya maji ya Kitaifa uzalishaji ni lita
milioni 59.5 ikilinganishwa na mahitaji ya lita 119 kwa siku, sawa na 50% ya
mahitaji” Alisisitiza Dkt. Mpango
Alibainisha kuwa vifo vitokanavyo na uzazi ni 556 katika kila vizazi hai 100,000
wakati lengo ni kuvipunguza visizidi vifo 265 katika kila vizazi hai 100,000
itakapofika mwaka 2020.
Aidha Dkt. Mpango alisema kuwa huduma za msingi
zinazotolewa na Serikali hususan, ulinzi wa nchi, usalama wa raia, na mali zao,
utawala, usimamizi wa rasimali za nchi, na ujenzi wa miundombinu ya msingi
isiyo na mvuto kwa sekta binafsi, lazima
ziendelee kugharamiwa na Serikali.
Dkt. Mpango alielezea pia namna misaada na mikopo kutoka
kwa wadau wa maendeleo inavyopungua mwaka hadi mwaka ambapo alisema mikopo
yenye masharti nafuu ilishuka kutoka shilingi trilioni 1.3 mwaka 2013/14 hadi
shilingi bilioni 495 mwaka 2015/2016
Alifafanua kuwa misaada kutoka kwa washirika hao
wa maendeleo imeshuka kutoka shilingi trilioni 1.5 kwa mwaka 2013/2014 hadi sh.
Trilioni 1.23 mwaka 2015/2016.
Vilevile alieleza kuwa kiwango cha ulipaji kodi
kwa hiari miongoni mwa wafanyabiashara na wawekezaji bado hakiridhishi na
ukwepaji kodi/uvujaji wa mapato ya Serikali bado ni matatizo sugu hivyo kuitaka
Sekta Binafsi iyatupie macho mambo hayo wakati wakijadili na kushauri namna
Serikali inavyoweza kuboresha kodi ili mambo hayo ya msingi ya kuihudumia jamii
yasikwame
Wakizungumza kwa niaba ya Sekta
Binafsi, Mwenyekiti wa Shirikisho la wenye viwanda hapa nchini Dokta Samuel
Nyantahe na mmoja wa wafanyabiashara Bw. Boaz Ogola, wameishukuru Serikali ya
awamu ya tano kwa nia yake ya dhati ya kuboresha mazingira ya uwekezaji na
ufanyaji biashara hapa nchini na kwamba wako tayari kushirikiana nayo ili
kutimiza azma yake ya kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kwa kuwa
wameiona nia njema ya Serikali ya kufikia hatua hiyo
Mkutano huo wa siku moja
umewakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi huku
agenda kuu ya mkutano huo ilikuwa kujadili kwa undani masuala mbalimbali ya
kodi ambapo Sekta binafsi imependekeza mambo kadhaa ambayo Serikali imeahidi
kuyafanyiakazi.
Post a Comment
karibu kwa maoni