Zanzibar wamefuzu kwa fainali ya
ubingwa wa kanda ya Afrika mashariki na kati, maarufu kama Cecafa Senior
Challenge baada ya kuwalaza Uganda Cranes 2-1.
Zanzibar Heroes sasa watakutana na Kenya kwenye fainali Jumapili.Zanzibar walifunga mwanzo kupitia Abdul Azizi Makame dakika ya 25 kisha Derrick Nsibambi akatuliza kimiyani bao la Uganda la kusawazisha naye Mohammed Issa Juma akapachika wavuni bao la pili la Zanzibar .
Ni mara ya kwanza kwa Zanzibar kufika fainali michuano hiyo tangu 1995, mwaka ambao walitwaa ubingwa.
Allan Katerega wa Uganda anasema kuondolewa kwa Joseph Nsubuga kuliipunguzia nguvu timu yao.
Nsubuga alionyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu Feisal Salum Abdulla wa Zanzibar.
Wenyeji Kenya walifuzu baada ya kuwashinda Burundi kwa bao la muda wa ziada lililofungwa na kiungo wa kati Whyvonne Isuza.
Katibu mtendaji wa baraza la taifa la michezo Zanzibar Khamis Ali Mzee tayari amesema: "Sasa Fifa wapende wasipende watatutambua."
Zanzibar si wanachama wa Fifa licha ya kupigana kwa muda mrefu watambuliwe.
Wanajumuishwa wote pamoja na Tanzania bara.
Lakini Ali asema ndugu mkubwa hawapi fungu lao kutoka Fifa.
"Nitasema hapo tumefinywa lakini tutafanikiwa siku moja."
"Walijaribu kutuzuia CAF tusishiriki michuano hii ya Cecafa lakini ndugu mkubwa akatutetea tena tuliwaambia sisi ni baadhi ya waanzilishi miaka hiyo ikiwa Gossage Cup," asema Ali.
Post a Comment
karibu kwa maoni