0
Mkuu wa Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara, Chelestino Mofuga amemuagiza Mkuu wa Polisi wilayani humo kumkamata Eliud Petro (50) akituhumiwa kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais.

Mofuga ametoa kauli hiyo jana Jumanne Januari 23,2018 akitaka Petro akamatwe na kuwekwa ndani kwa saa 48 na baadaye kufikishwa mahakamani.

Amesema mtuhumiwa alitumia lugha hiyo baada ya kukamatwa na polisi kwa kosa la kuvamia eneo la Shule ya Msingi Endamasak na kulima.

Mofuga amesema wakati polisi wakiendelea kuwakamata wenzake wanne, Petro alitamka kuwa Rais John Magufuli naye ni mtuhumiwa bila kufafanua anatuhumiwa kwa kosa gani.

Amebainisha kuwa Petro na wenzake walikamatwa kwa kosa la kuvamia na kulima eneo la shule hiyo.

Amewataja watuhumiwa wengine kuwa ni Yohana Baida, Boay Nonash, Paulo Gutii na Martin Joseph.

Mofuga amesema kwa mamlaka aliyonayo amemuagiza mkuu wa polisi wa wilaya  kumweka rumande kwa saa 48 mtuhumiwa na kumfikisha mahakamani.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top