0
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema askari wanaotembea na pikipiki maarufu kama ‘tigo’ hawana mamlaka ya kutoza faini kwa mtu aliyevunja sheria za barabarani.

Amesema jukumu lao ni kumkamata aliyevunja sheria na kumpeleka kwa askari wa usalama barabarani.

“Niwasihi wananchi,  msikubali kutoa hela kwa hao askari hiyo itakuwa ni rushwa. Fedha unayompa inamfaidisha askari husika na familia yake. Jambo hili tunalipinga mno,” amesema Mambosasa leo Januari 18, 2018 katika kipindi cha 360 kinachorushwa na Redio Clouds.

Amesema kikosi hicho cha pikipiki hakikuanzishwa kwa ajili ya kukamata wanaovunja sheria barabarani na kuwatoza faini, kwamba askari wa usalama barabarani ndio wenye jukumu la kutoza faini na kutoa risiti.

“Kikosi cha pikipiki kilianzishwa kwa ajili ya kuangalia usalama na inapotokea kosa wanawajibika kumfikisha mhusika kwenye mamlaka inayosimamia usalama barabarani,” amesema.

Ametoa wito kwa askari wa usalama barabarani kutumia busara wakati wa kuteleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.

“Tunaelekeza polisi asitafute makosa, asikusimamishe bila kujua kwanini amekusimamisha halafu anaanza kuhangaika kutafuta kosa. Tunaendelea kuwaeleza wenzetu kuwa busara inahitajika wakati wa kusimamia sheria,” amesema na kuongeza,

“Hawapaswi kuwaumiza watu. Askari unatakiwa kufikiria tu unamtoza faini mtu mchana kwa kuwa taa zake haziwaki sasa hapo anakuwa amefanya kosa gani maana ametembea mchana, labda ingekuwa usiku halafu taa haziwaki hapo sawa.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top