0
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira imeaigiza Serikali kuchukua hatua za haraka, kuruhusu kuondolewa kwa sukari ya viwandani iliyokwama Bandari ya Dar es Salaam ili kuvinusuru viwanda vitano vilivyo hatarini kufungwa kwa kukosa malighafi hiyo.
Imetoa agizo hilo baada ya mjadala mkali kuibuka katika kikao chake mjini hapa, baada ya hoja iliyowasilishwa na viwanda hivyo kupitia Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI). Mwenyekiti wa CTI, Samwel Nyantae aliiambia kamati kuwa viwanda vya Coca-Cola Kwanza Limited cha Dar es Salaam, Sayona cha Dar es Salaam na Mwanza, Ivory cha Iringa, Iringa Food Beverage na Anjari cha Tanga, viliwasilisha malalamiko yao kwa kamati hiyo vikidai kuwa vipo hatarini kufungwa, kwa kukosa sukari wanayoitumia kuzalishia bidhaa.
Akizungumza na vyombo vya habari baada ya agizo hilo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Mvomero, Sadick Murad (CCM) alisema wameiagiza Serikali kuchukua hatua za haraka kuvinusuru viwanda kufungwa na kuathiri ajira za mamia ya wafanyakazi wao.
“Hoja zao ni kuwa wanavyo vibali vya kuagiza sukari hii ya viwandani na walishaagiza sukari kulingana na vibali vyao, lakini sukari hiyo imekwama bandarini Dar es Salaam na wanapouliza hawapewi majibu ya uhakika.
Sasa suala la viwanda lipo chini ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, lakini la misamaha ya kodi kwa sukari ya viwandani lipo chini ya Waziri wa Fedha na Mipango na vibali vya sukari vipo chini ya Sudeco (Shirika la Maendeleo ya Sukari) lililo Wizara ya Kilimo.
“Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji (Charles Mwijage) alikuwepo hapa kwa hiyo tumempa muda hadi kesho (leo) awe amekutana na mawaziri wenzake ili kupata ufumbuzi wa suala hili,” Murad aliwaambia waandishi habari.
Alisema kamati yake imebaini baadhi ya maofisa wa serikali, wametafsiri vibaya agizo la Rais John Magufuli kutaka mamlaka za utoaji wa vibali vya kuingiza nchini, kuhakiki shehena ya sukari ya viwandani kabla ya kutoa vibali.
Alisema Rais alitoa agizo hilo, baada ya kuwepo malalamiko ya viwanda vinavyozalisha sukari kuwa sukari ya viwandani inayoingizwa nchini kwa uzalishaji viwandani, imekuwa inauzwa mitaani na wafanyabiashara wasio waaminifu na kuathiri soko la sukari ya kawaida inayouzwa.
“Rais alichoagiza na mimi kama Mwenyekiti nilikuwepo ni kuwa maofisa wanaohusika na utoaji wa vibali vya uagizaji sukari ya viwandani, wafanye uhakiki wa kutosha ili kujiridhisha mahitaji ya waagizaji kabla ya kuwapa vibali ili sukari hiyo iingizwe kulingana na mahitaji ya viwanda.
“Sasa Kamati imebaini kuwa baadhi ya maofisa wanakwamisha uingizaji wa sukari kwa matumizi ya viwanda kwa sababu ambazo ni tofauti na maagizo ya Rais na ndiyo maana tumewapa muda mfupi ili waweze kuleta majibu kwa kamati yetu na sisi kuwasilisha bungeni,” alisema Murad.
Alisema wamefikia uamuzi huo ili kuhakikisha viwanda hivyo, vinaendelea na uzalishaji, hatua ambayo pamoja na kuipatia serikali mapato itaokoa pia ajira za wananchi wengi masikini ambao wameajiriwa katika viwanda hivyo.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top