0
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein akihutubia wananchi waliohudhuria sherehe za miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizofanyika Uwanja wa Abeid Amani Karume kisiwani Zanzibar jana. Kushoto ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli. (Picha na Ikulu).RAIS Ali Mohamed Shein wa Zanzibar ametangaza kwamba kuanzia Julai mwaka huu, michango yote iliyokuwa ikitolewa na wazazi katika elimu ya sekondari visiwani Zanzibar itafutwa.
Amesema hatua hiyo inachukuliwa kutokana na kuimarika kwa uchumi na ukusanyaji wa mapato na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) inakusudia kuimarisha huduma za afya na elimu.
“Natangaza rasmi kufuta michango yote iliyokuwa ikitolewa na wazazi kwa ajili ya kugharamia elimu ya sekondari kwa wanafunzi wa Unguja na Pemba... natangaza kufuta michango yote ifikapo Julai mwaka huu,” alisema Dk Shein akihutubia Taifa kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar jana.
Huku akishangiliwa na mamia ya wananchi waliofurika kwenye Uwanja wa Amaan mjini Unguja, Dk Shein alisema uamuzi huo unakwenda sambamba na kutekeleza dhamira ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume aliyetangaza elimu bure kwa wananchi wote.
Tayari kwa upande wa michango ya wanafunzi wa elimu ya msingi, michango yote imefutwa miaka miwili iliyopita huku elimu ya maandalizi (ya awali) ikifanywa kuwa ya lazima. Aidha, Dk Shein amesema Mapinduzi ya Zanzibar yamepata mafanikio makubwa katika sekta ya maendeleo na kiuchumi na kusisitiza serikali yake itayalinda kwa nguvu zote.
Alisema Mapinduzi ndiyo yaliyoleta usawa wa wananchi wa Unguja na Pemba kutoka katika ukandamizaji wa watawala wa kisultani kutoka Oman. Alieleza kwamba wakati wananchi wakiadhimisha miaka 54 ya Mapinduzi, hakuna mtu ambaye hajafaidika na faida na matunda ya Mapinduzi hayo yaliyoenziwa hadi leo.
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kulinda na kuyatunza mapinduzi ya Zanzibar ambayo yameleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi na maendeleo kwa wananchi wake na hizo ndiyo faida ya Mapinduzi,” alisema Dk Shein katika sherehe ambazo pia zilihudhuriwa na Rais John Magufuli.
Akielezea hali ya ukusanyaji wa mapato, alisema SMZ imepiga hatua kubwa kupitia taasisi zake za kodi Zanzibar (ZRB) na Tanzania (TRA) ambapo jumla ya Sh bilioni 548.57 zilikusanywa katika mwaka 2017 ukilinganishwa na Sh bilioni 487.474 zilizokusanywa katika mwaka 2016.
Alisema mapato yameongezeka Sh bilioni 61.097 ikilinganishwa na makusanyo ya mwaka 2016 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 12.5. Aliongeza kuwa Pato la Taifa limeongezeka kutoka Sh bilioni 2,308 katika mwaka 2015 na kufikia Sh bilioni 2,628 katika mwaka 2016 huku matarajio zaidi kuongezeka na kufikia Sh bilioni 2,827 mwaka 2017.
Alisema uchumi wa Zanzibar umekua na kufikia asilimia 7 katika mwaka 2017 ukilinganisha na asilimia 6.8 mwaka 2016 huku akisifu mazingira ya amani na utulivu kuwa umesaidia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa mazingira hayo.
Mapema, Dk Shein alitoa ahadi ya kuendelea kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao umekuja kutokana na Mapinduzi ya Januari 12, 1964. Alisema yapo mafanikio makubwa yamepatikana katika miradi ya Muungano inayotekelezwa na serikali mbili huku akiutaja mpango wa kunusuru kaya masikini, Tasaf, kuwa umekidhi malengo ya watu waliokusudiwa.
Kwa mfano, alisema jumla ya kaya 32,478 zimefikiwa katika mpango wa kunusuru kaya masikini ambapo umetumia jumla ya Sh bilioni 4.45 huku ukisaidia kutoa ajira za muda kwa walengwa wake.
“Miongoni mwa miradi inayotekelezwa ya muungano ni Tasaf ambao umepiga hatua kubwa na kunusuru kaya masikini zipatazo 32,478 ikiwemo kutoa ajira za muda kwa walengwa,” alieleza.
Mamia ya wananchi walianza kuingia mapema kwenye Uwanja wa Amaan kuanzia saa 12 ambapo sherehe hizo zilimalizika mapema saa 5.30 kwa ajili ya kutoa nafasi Waislamu kuhudhuria ibada ya sala ya Ijumaa.
Sherehe za miaka 54 zilihudhuria na viongozi wote wakuu wa kitaifa wakiwemo marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano, mawaziri wakuu na mawaziri kutoka Serikali ya Muungano na Zanzibar.
Walikuwapo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete, Amani Abeid Karume, Makamu wa Rais mstaafu Dk Mohamed Gharib Bilal, na viongozi wengine mbalimbali.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top