0
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo  amesema Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema wanamuonea wivu waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa kwa kupata nafasi ya kuongea na Rais John Magufuli.

Lowassa jana Jumanne alitembelea Ikulu ya Dar es Salaam na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli ambapo pamoja na mambo mengine alimpongeza Rais kwa jitihada zake za kuleta maendeleo na ajira kwa vijana.

Hatua hiyo ya Lowassa ilikosolewa na baadhi ya viongozi wakubwa wa chama chake wakieleza kuwa hakutakiwa kutoa pongezi kwa Rais huyo kwa kuwa uongozi wake una kasoro huku wakiuambia umma kwamba maneno ya Lowassa ni ya kwake binafsi na sio msimamo wa chama chake.

 Gambo ambaye awali alijinadi kuwa Lowassa anamuomba amuombee nafasi ya kuonana na Rais, amesema wanaokosoa wanafanya hivyo kwa kuwa wao hawajabahatika.

"Lowassa alikuwa na kiu ya muda mrefu kutaka kumuona Rais hatimaye Rais amemaliza kiu hiyo. Mbowe na Lema nao kama watu wenye akili timamu bila shaka nao wanayo kiu ya kuonana na kiongozi mkuu wa nchi, hivyo niwatake wafuate taratibu na kama Rais atakuwa na nafasi ataonana nao hana shida katika hilo," amesema Gambo.

Amesema  Rais ameonyesha mfano wa siasa safi na vijana wanapaswa kuiga mfano wake kwani baada ya uchaguzi agenda yake kubwa ni maendeleo.

Alipoulizwa kuwa tukio la jana ni matokeo ya matamshi yake ya kutumwa na Lowassa ambayo baadaye Lowassa mwenyewe aliyakana, Gambo amesema "Ninaloweza kusema ni Rais kamaliza kiu ya muda mrefu."

Kuhusu kama kweli ujumbe huo aliufikisha kwa Ikulu kwa Rais Magufuli Gambo amesema " Mawasiliano ya Rais na Mkuu wa Mkoa si jambo la umma hivyo nisilizungumzie,"

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top