0
ASKOFU Msaidizi wa Jimbo Katoliki Bukoba Mhashamu Methodius KilainiWANANCHI wametakiwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa katika kipindi cha mwaka 2018, ili kuondokana na kile kinachodaiwa kuwa hali ngumu ya maisha.
Wanasiasa, wasomi na viongozi wa dini wametoa ushauri kwa wananchi kwamba njia pekee ya kuondokana na maisha magumu kwa mwaka 2018 ni kufanya kazi.
Mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Razack Lokina alisema kuwa wananchi wanapaswa kuelewa kwamba hakuna pesa pasipo kufanya kazi. Alisema mtindo wa maisha wa kukaa vijiweni wa baadhi ya watu, lazima ubadilike na wajikite kwenye kufanya kazi.
“Kuna baadhi ya watu waliishi kwa kutegemea biashara za madawa ya kulevya au rushwa, mambo hayo kwa sasa yamedhibitiwa, njia pekee ni kufanya kazi la sivyo maisha yatakaza tu,” alisema Profesa Lokina.
Hoja hiyo ya wananchi kufanya kazi kwa bidii, imeungwa mkono na Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini. Askofu Kilaini alisema kuwa baadhi ya wananchi walikuwa na fedha nyingi lakini wakajisahau kufanya mambo ya maendeleo, na hivyo kufanya maisha yao kuwa magumu.
Alisema kuwa njia pekee ya wananchi kuondokana na ugumu huo wa maisha kwa mwaka 2018 ni kujifunga mkanda na kufanya kazi kwa bidii. “Baba (Rais John Magufuli) ameamua kujenga nyumba, hivyo fedha haziwezi kuendelea kubaki mifukoni.
“Fedha zimeelekezwa kwenye kuleta maendeleo halisi kama vile kuboresha huduma za jamii ikiwemo elimu, afya, ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli ya kisasa, ununuzi wa meli na ndege; hayo yote hayawezi kufanyika bila kutumia fedha,” alieleza Askofu Kilaini.
Kwa mujibu wa Askofu Kilaini, kitendo cha Serikali kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma, zilizokuwa zikitumika kwa kulipana posho mbalimbali, nacho kimechangia kufanya maisha ya baadhi ya watu kuwa magumu. Alisema kuzibwa kwa mianya hiyo, kumeisaidia Serikali kuelekeza fedha kwenye shughuli za maendeleo.
Kwa upande wake, Profesa wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Prosper Ngowi alisema ugumu wa maisha ambao wananchi wadai kukumbana nao, unapaswa kutazamwa kwa pande mbili ambazo ni wananchi wenyewe na upande wa pili ni Serikali.
Profesa Ngowi alisema kwa upande wa wananchi hali ngumu inaweza kuwa imesababishwa na vyanzo vyao vya mapato kupotea. Alisema ili kuondokana na hali hiyo, wananchi wanapaswa kuvibaini vyanzo hivyo na kuvirejesha ili kuendelea kujiingizia kipato.
\Kwa upande wa Serikali, Profesa Ngowi alisema inapaswa kuangalia sera zake za ajira na mikopo zikoje. Alisema wananchi wengi hawana mitaji na ajira, hivyo kama serikali itaweka sera nzuri za kuwasaidia wananchi kupata mikopo na ajira itawasaidia kuondokana na ugumu wa maisha wanaodai kukumbana nao.
Pamoja na ushauri uliotolewa kwa wananchi kufanya kazi kwa bidii, Mwenyekiti wa chama cha UPDP, Fahim Dovutwa alisema kuwa wananchi bado hawajaelewa mwelekeo wa Rais Magufuli pamoja na kuwa amekuwa akiwasisitiza kufanya kazi kwa bidii.
Alisema ili kuondokana na hali hiyo ya ugumu wa maisha, viongozi mbalimbali wanatakiwa waendelee kuwaelimisha wananchi kuhusu mwelekeo wa serikali. Alisema pamoja na wananchi kumuunga mkono kwa hatua anazochukua dhidi ya mambo mbalimbali kama vile ufisadi, lakini bado hawajaelewa vizuri

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top