Madiwani
watatu wa Chadema, katika halmashauri ya Longido mkoa wa Arusha ,
wametangaza kujiuzulu na kujiunga na Chama cha Mapinduzi ( CCM).
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Longido, Jumaa Mhina alithibitisha
leo Januari 10 kujiuzulu kwa madiwani hao, Jacob Silas Mollel Kata ya
Elang'atadapash, Elias Mepukori Mbao Kata ya Kamwaga na Diyoo Lomayani
Laizer Kata ya Olmolog.
Mhina amesema sababu za kujiuzulu madiwani hao wamezitoa kuwa ni kuunga
mkono jitihada za Rais John Magufuli katika vita dhidi ya ufisadi,
kuinua uchumi na pia kurejesha nidhamu kazini.
"Tayari tumepokea barua zao na tumezipeleka TAMISEMI kwa ajili ya
utaratibu wa kisheria ili kuwezesha kufanyika uchaguzi mdogo baada ya
Tume kupata taarifa" Amesema
Aliyekuwa mbunge wa jimbo la Longido, Onesmo ole Nangole pia
amethibitisha kuondoka kwa madiwani hao na kueleza chama hicho,
kinafuatilia tukio hilo.
Madiwani hao kujiunga na CCM wanafanya mkoa wa Arusha pekee kuwa na
jumla ya madiwani 13 wa Chadema ambao wamejiuzulu na kujiunga na CCM
tangu kumalizika uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Post a Comment
karibu kwa maoni