0
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufaa, Semistocles KaijageWANANCHI wa majimbo ya Singida Kaskazini, Songea Mjini na Longido pamoja na kata tano nchini, wanapiga kura katika Uchaguzi Mdogo kwa ajili ya kuwachagua wabunge na madiwani katika nafasi zilizoachwa wazi.
Katika uchaguzi huo, jumla ya vituo 742 vya ubunge vitahusika kupigia kura huku kwa kata tano ni vituo 856. Kwa Jimbo la Singida Kaskazini mkoani Singida, uchaguzi huo unafanyika kuziba nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wake, Lazaro Nyalandu aliyefukuzwa uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwishoni mwa mwaka jana kisha kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Jimbo la Longido mkoani Arusha wanachagua mbunge kutokana na maamuzi ya Mahakama Kuu kutengua ushindi wa Mbunge wa Chadema, Onesmo Ole Nangole ambaye alishindwa katika rufaa mbalimbali. Jimbo la Songea Mjini mkoani Ruvuma liko wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa mbunge, Leonidas Gama.
Aidha, kata tano zitakazohusika katika uchaguzi wa madiwani ni Keza iliyoko Halmashauri ya Ngara, Kimandolu ya Halmashauri ya Jiji la Arusha, Kurui ya Kisarawe, Bukumbi ya Tabora Uyui, na Kwagunda wilayani Korogwe.
Kata ya Kihesa iliyopo Iringa, mgombea wake amepita bila kupingwa, hivyo haitoshiriki katika uchaguzi huo. Katika uchaguzi huo mdogo, vyama vilivyojiorodhesha kushiriki ni Ada Tadea, AFP, CCM, Demokrasia Makini, NRA, Sauti ya Umma (SAU), TLP, Chama cha Wananchi (CUF), CCK, DP, na UPDP.
Hata hivyo, Chadema kimejitoa kushiriki katika uchaguzi huo mdogo kwa madai yakuwepo kwa fujo na baadhi ya wagombea na wananchi kupigwa pamoja na kukosekana kwa demokrasia.
Akizungumzia uchaguzi huo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Semistocles Kaijage alisema wapiga kura watatumia daftari la wapiga kura la mwaka 2015 na wale waliopoteza kadi za kupigia kura, kuharibika ama kuchakaa, watapiga kura kwa kutumia vitambulisho vya Taifa, pasipoti ama leseni ya udereva.
Hata hivyo, alisema ili wapiga kura hao washiriki vyema katika uchaguzi huo, sharti majina yao yawemo katika daftari la kupigia kura la mwaka huo na kwa eneo husika.
Alisema ili anayehusika aruhusiwe kutumia vitambulisho hivyo ni sharti awe aliandikishwa kwenye daftari la wapiga kura mwaka 2015, jina lake liwe katika orodha ya wapiga kura katika kituo anachokwenda kupiga kura na majina yake yaliyomo katika daftari yafanane kwa herufi, maneno na tarakimu na majina yaliyopo katika kitambulisho atakachotumia badala ya kadi ya kupigia kura.
Hata hivyo, alisema Tume iko katika maandalizi ya awali ya uboreshaji wa daftari hilo, kwani tangu kukamilishwa kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 haijaboresha, hivyo kwa mujibu wa vifungu 13( 2) na 61 (3) (a) vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na kifungu cha 62 (a) cha Sheria ya Uchaguzi za Serikali za Mitaa imeruhusu wapiga kura walioandikishwa mwaka 2015.
Alivitaka vyama vitakavyoshiriki uchaguzi huo kuheshimu, kuzingatia na kutekeleza sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi, maadili ya uchaguzi, maelekezo ya Tume pamoja na sheria zingine za nchi kwa wakati huo wa uchaguzi.
Mkoani Singida, Msimamizi wa Uchaguzi katika Jimbo la Singida Kaskazini ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Rashid Mandoa alisema maandalizi yote muhimu ya uchaguzi huo yamekamilika ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa vifaa vya kutosha kwa shughuli nzima.
Alivitaja vyama vitakavyoshiriki kuwa ni CCM, CCK, Ada Tadea, CUF na AFP na jumla ya wapiga kura 91,562 wanatarajiwa kupiga kura kwenye vituo 246 vilivyopangwa. Katika Jimbo la Longido, Msimamizi wa Uchaguzi, Juma Mhina alisema uchaguzi huo unahusisha vyama tisa vya siasa ambavyo vilivyojitokeza na kufanikiwa kukamilisha vigezo.
Mhina ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, alisema jimbo la Longido lina kata 18 na vituo 175 vya kupiga kura na waliojiandika kupiga kura katika jimbo hilo ni wananchi 57,808.
Katika Jimbo la Songea Mjini, jumla ya wapiga kura 45,000 kati ya 127,000 wanatarajia kupiga kura leo. Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Songea Mjini, Tina Sekambo alisema vyama vitatu vitashiriki uchaguzi huo ambavyo ni CCM, ADA Tadea na CUF.
Aidha Sekambo, amewataka wakazi wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi leo kwa ajili ya kupiga kura na kusema kuwa maandalizi yote ya uchaguzi yamekamilika ikiwemo karatasi za kupigia kura. Imeandikwa na Lucy Lyatuu (Dar), John Mhala (Longido), Abby Nkungu (Singida) na Muhidin Amri (Songea).

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top