0
IDADI ya madiwani wa Jimbo la Iringa Mjini waliochaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) inazidi kuputika baada ya diwani mwingine, Oscar Kafuka wa Kata ya Mkwawa kutangaza kujiuzulu juzi usiku.
Kafuka anakuwa diwani wa sita kubwaga manyanga katika kipindi cha miezi minne iliyopita kutokana na sintofahamu ya uongozi inayoendelea ndani ya chama hicho. Kujiondoa kwa madiwani hao kunaifanya Chadema iliyonyakua viti 14 kati ya 18 vya udiwani katika jimbo hilo mwaka 2015 na kubeba Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, kubakiwa na madiwani nane ambao pia hakuna mwenye uhakika kama wote wataendelea kuzitumikia nafasi hizo hadi mwaka 2020 utakapofanyika Uchaguzi Mkuu mwingine.
Wakati Chadema ikibakiwa na madiwani nane wa kuchaguliwa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa upande wake kimeongeza idadi ya madiwani kutoka wanne hadi sita, baada ya kushinda katika Uchaguzi Mdogo katika kata ya Kitwiru na mgombea wake kupita bila kupingwa katika Kata ya Kihesa iliyokuwa ifanye uchaguzi leo.
Aidha, CCM inatarajia kushinda katika kata zingine nne zilizo wazi hasa kwa kuwa Chadema kwa kupitia Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe ilikwishatangaza kutoshiriki uchaguzi mdogo wowote kwa madai kwamba chaguzi hizo haziko huru na haki; jambo litakaloifanya iwe katika nafasi nzuri ya kuongeza madiwani wake hadi 10.
Tarifa za kujiuzulu kwa madiwani wa Chadema zinazidi kupokelewa kwa nderemo na vifijo na wanachama na viongozi wa CCM. Mwenyekiti wa CCM wa Manispaa ya Iringa, Said Rubeya alisema;
“Hatukuamini macho yetu tulipopoteza jimbo na halmashauri katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 na sasa hatuamini macho yetu jinsi yanavyoshuhudia madiwani wa Chadema wakijiengua katika chama hicho.”
Rubeya alisema kwa maamuzi hayo ya madiwani wa Chadema, CCM inajiona ipo katika mazingira mazuri ya kuirudisha Halmashauri ya Manispaa ya Iringa katika mikono yake.
“Endapo Chadema itapoteza madiwani wengine wawili, hakuna shaka meya wa sasa atakuwa amepoteza mamlaka ya kuendelea kukikalia kiti hicho na hivyo Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Iringa litalazimika kuchagua meya mwingine na endapo itakuwa hivyo hakuna shaka CCM watakuwa katika nafasi nzuri ya kutwaa kiti hicho,” alisema Rubeya.
Akizungumzia hamahama ya madiwani wao na hatma yake, Meya wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe alisema jambo hili linawaumiza wapenda mageuzi wengi kwani walipowachagua madiwani kutoka upinzani hawakujua kama hatma yake itakuwa kutoswa katikati ya njia.
“Walipoanza kuondoka na kujiunga na CCM, tumekuwa tukifanya vikao, bahati mbaya madiwani wanaohama, wamekuwa wakiapa mbele ya vikao kwamba hawana sababu na hawawezi kufanya hivyo. Lakini yanayotokea ndiyo hayo,” alisema Kimbe.
Akiwa Meya wa manispaa hiyo alisema anaiona dalili ya kupoteza kiti hicho kwa CCM, lakini alijipa moyo akisisitiza; “sikuzaliwa kuwa meya na kwamba hayo ni majukumu ya kupokezana ambayo matokeo yake huamriwa kwa kura.”
“Ombi kwa wanamageuzi wenzangu, tusikate tamaa, kuna kimbunga cha ajabu kinapita katika chama chetu, tukumbuke hakuna jambo lisilo na mwisho, nina hakika mambo yatakaa sawa,” alisema huku akisisitiza kwamba hafikirii kuhama chama hicho kama walivyofanya madiwani wenzake na akawaomba pia wenzake waliobaki wasiwakimbie wapiga kura wao kwa kuhama chama hicho.
Akizungumza na wanahabari juzi, diwani aliyejiuzulu alisema; “Nimeamua kujiuzulu kwa hiari yangu mwenyewe baada ya kuona napoteza muda mwingi katika nafasi hii na kwa kuzingatia ahadi nyingi nilizotoa wakati wa uchaguzi mkuu uliopita sasa zinatekelezwa na serikali ya Dk John Magufuli kwa kasi kubwa.”
Kwa muktadha huo, Kafuka alisema haoni tena sababu ya kuendelea na wadhifa huo na kujishughulisha na mambo ya kisiasa kwa sasa na badala yake anataka kuitumia familia yake na kuendeleza shughuli zake za ukandarasi zilizoanza kuyumba baada ya kuwa diwani.
“Nichukue nafasi hii kuwashukuru wananchi wa kata yangu na manispaa ya Iringa kwa ushirikiano walionipa katika kipindi nilichokuwa diwani wao na kufanikiwa kutekeleza majukumu mbalimbali ya kuwaletea maendeleo,” alisema

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top