0
Waziri wa Fedha na Mipango, Philip MpangoSerikali imeamua kufanya mazungumzo na kampuni ya simu ya Airtel kuhusu umiliki wa kampuni hiyo ili nchi iweze kupata haki yake, baada ya Kamati iliyoundwa kuchunguza umiliki wa kampuni hiyo kubaini ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na taratibu.
Serikali inayomiliki asilimia 40 itafanya mazungumzo na kampuni ya Airtel inayomiliki asilimia 60 za hisa za kampuni hiyo ili nchi iweze kupata haki yake inayostahili.
Waziri wa Fedha na Mipango ameyasema hayo baada ya kuwasilisha taarifa ya kamati aliyoiunda kuchunguza sakata hilo kwa Rais John Magufuli ambapo amesema, serikali imepoteza fedha nyingi, hivyo katika majadiliano hayo yatakuwa na lengo la kuhakikisha Watanzania wanapata haki yao.
“Lakini niwaambie Watanzania yale ambayo tumeyaona ni machafu sana, ni mambo ya hovyo kabisa, nchi yetu kwa kifupi tuliingizwa mkenge, ni fedha nyingi zimepotea kwa hiyo sisi katika majadiliano haya lengo letu litakuwa ni kuhakikisha Watanzania wanapata haki yao” amesema Dk. Mpango. 
Kamati ya kuchunguza sakata hilo, iliundwa na Dk. Mpango kutokana na agizo la Rais Magufuli alilolitoa Desemba 20, mwaka jana wakati akizindua jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), mjini Dodoma.
Katika taarifa ya kamati hiyo imebainisha kuwa ubinafsishaji wa Shirika la Simu Tanzania (TTCL) kwenda Celtel na baadae kuhamshiwa Zain na sasa Airtel ulifanyika kwa ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na taratibu.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top