0
Taarifa za Klabu ya Simba kumpa ajira kocha mpya zimeendelea kushika kasi na inaelezwa kuwa klabu hiyo ipo njiani kumshusha raia wa Ufaransa kukinoa kikosi chao.
Inaelezwa kuwa Simba ipo katika hatua hizo za mwisho kumleta nchini Tanzania, Hubert Velud ambaye ni kocha wa zamani wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) pamoja na Etoile du Sahel ya Tunisia.
Kocha huyo pia amewahi kumfundisha Emmanuel Adebayor katika kikosi cha timu ya taifa ya Togo, hivyo kwa ufupi ni kocha mwenye wasifu mkubwa na mzoefu wa soka la Afrika.
Habari kutoka ndani ya Simba zimesema kwamba, Velud mwenye umri wa miaka 58 anatararajiwa kutua nchini muda wowote kuanzia leo na anayehusika kwa ukaribu kumleta nchini ni Mohamed ‘Mo’ Dewji ambaye anatarajiwa kuwa sehemu ya wamiliki wa klabu hiyo.
Velud pia alikuwa kocha wa timu ya taifa ya Togo na alipigwa risasi mkononi wakati basi la wachezaji liliposhambuiliwa na waasi nchini Angola wakati wanakwenda kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2010.
Kocha huyo ana uzoefu wa kufundisha timu nyingi zikiwemo Gap, Paris FC, Gazelec Ajaccio, Clermont, Cherbourg, Creteil zote za Ufaransa.
Pia aliwahi kubeba taji katika timu ya ES Setif ya Algeria, akiwa nchini humo pia amewahi kuifundisha USM Alger .
Ujio wake Simba ni kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Mcameroon, Joseph Marius Omog aliyefukuzwa Desemba, mwaka jana.
Velud aliyezaliwa Juni 8, mwaka 1959 enzi zake alikuwa kipa, alianza kucheza soka mwaka 1976 hadi 1990 alipostaafu na kugeukia ukocha.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top