0
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba.WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba amesema kuwa wanatarajia uandikishaji wa wananchi kwenye Vitambulisho vya Taifa (NIDA) utakapokamilika, vitambulisho hivyo vitumike kwa ajili ya kupigia kura.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa Mkoa wa Ruvuma hivi karibuni, Dk Nchemba alisema kuwa hata kama wananchi watakuwa na vitambulisho vitano vya kupigia kura, vitakuwa batili kama mtu hatakuwa na kitambulisho cha uraia.
Alisema kuwa serikali inaendelea kufanya maboresho ya mifumo mbalimbali ya vitambulisho vya uraia na kwamba itakapokaa vizuri, vitatumika kupigia kura. ‘’ Vitambulisho vyote ulivyojiandikisha vya kupigia kura hata kama unavyo vitano vitakuwa batili kama hutakuwa na kitambulisho cha uraia, tunategemea kuwa kitambulisho cha Taifa ndicho kitatumika kupigia kura hivyo uandikishaji unapaswa kuwa na ufanisi mkubwa kama inavyotarajiwa,’’ alisema Dk Nchemba.
Pia alisema baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa, wanaowadai wananchi michango kwa ajili ya kupata vitambulisho hivyo, wanapaswa kuchukuliwa hatua kwa kuwa serikali imeshagharamia kila kitu ili watu wapate vitambulisho bure.
Alisisitiza kuwa mtu atakayekuwa hana kitambulisho baada ya uandikishaji kukamilika nchi nzima, maelezo yake yatakuwa magumu kueleweka kama yeye ni Mtanzania kweli na kueleza kuwa hata mtu akitoa sababu zipi hataeleweka.
Kaimu Mkurugenzi wa Nida, Andrew Masawe alisema kuwa baada ya kukamilika kwa uandikishaji wakazi wa mkoa huo, wanategemea kabla ya mwisho wa mwezi huu kuanza hatua hiyo katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Tabora na Kagera.
Alisema kwamba mikoa ya pembezoni itakayokuwa imebaki, kutakuwa na utaratibu maalum wa kufanya usajili. Alisema licha ya matarajio yao ya kukamilisha usajili wa vitambulisho hivyo Desemba 2018, wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo wananchi kushindwa kuambatanisha vitu muhimu vinavyoonesha umri, makazi na uraia.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme aliagiza wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na viongozi wa serikali za mitaa na vijiji, kusimamia uandikishaji huo kwa karibu ili utekelezaji uwe kwa vitendo na wananchi wajulishwe.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top