Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema hakielewi lengo la Jeshi
la Polisi mpaka sasa limekusudia kuwafanyia kitu gani viongozi wa
Chadema kwa madai wanaitwa kila uchao halafu hakuna kinachojadiliwa
kuhusiana na wito wao.
Hayo
yameelezwa jana mchana na Mkurugenzi wa Itifaki na Mawasiliano ya
Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema baada ya Mwenyekiti wa chama hicho
Freeman Mbowe na Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu kuhudhuria
kituo cha Polisi Jijini Dar es Salaam kama walivyotakiwa hapo awali
kufanya hivyo na mwishowe kuachiwa kurudi walipotoka bila ya kuhojiwa
jambo lolote lile tangu walipofika hapo majira ya asubuhi.
"Ni
kweli Mwenyekiti Freeman Mbowe na Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum
Mwalim waliripoti Polisi lakini hakukuwa na majadiliano ya aina yeyote
yaliweza kufanywa siku ya leo.
"Hatujui
mpaka sasa Jeshi la Polisi linatutakia nini, kwa maana ninavyojua watu
wakisha chukuliwa maelezo huwa Polisi wanaangalia kama watakuwa na kesi
ya kujibu au laa, na kama itakuwepo basi wanapelekwa Mahakamani na kama
hakuna basi jalada linafungwa. Sasa kwa upande wetu Jeshi la Polisi
halijafunga jalada wanasema bado uchunguzi unaendelea.
"Kwa
kweli sisi mpaka sasa hivi tunaona ni usumbufu na hii sio mara ya
kwanza maaana hata Mhe. Edward Lowassa aliwahi kuitwa polisi akawa
anahudhuria kila siku na mwisho wa siku hata hatujui lile jalada
lilipotelea wapi walilokuwa wamempa juu ya kutoa kauli za uchochezi
kwenye suala la Masheikh.
"Sasa
tunaona suala hili linajirudia kwa viongozi wetu wanaitwa kila siku,
hawapelekwi mahakamani, jalada halifungwi huku ni kuwafanyia watu
usumbufu kwa maana wengine ni wabunge kama Mbowe ametoka Mkoani Dodoma
ambapo walikuwa wanajadili mpango wa bajeti anaitwa kuja kuripoti
Polisi, sasa sijui gharama zote hizo nani atazilipa".
Kwa
upande mwingine, viongozi wa Chadema wametakiwa kuripoti tena Polisi
siku ya Alhamis (Machi 22, 2018) ambapo bado mpaka sasa haijafahamika
wanachoitiwa tena.
Post a Comment
karibu kwa maoni