Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amekutana na
kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Uchumi Mpana, Biashara na Uwekezaji wa
Benki ya Dunia, Dkt. Felipe Jaramilo katika ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango Dar es Salaam.
Katika kikao hicho, Waziri wa Fedha na Mipango aliishukuru
Benki ya Dunia kwa kuendelea kuisaidia Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa
na Dk. John Pombe Joseph Magufuli katika
kutekeleza miradi mbalimbali ya maedeleo hapa nchini.
Dkt. Mpango ameeleza kuwa uchumi wa nchi umeendelea kukua
kwa kiwango cha kati ya asilimia 6-7 kwa
muda na hivyo kuiwezesha Serikali kuendelea na utoaji wa huduma za jamii na
kuwekeza katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Dkt. Mpango ameeleza kuwa
pomaja na nia ya kuendeleza
mafanikio mazuri yaliyopatikana katika awamu za Serikali zilizopita, Serikali
ya Awamu ya Tano ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imedhamiria kwa dhati
kujenga uchumi imara kwa kuendeleza viwanda na kuweka mazingira mazuri ya
biashara ili kuvutia wawekezaji wa ndani na wale wa nje kuja kuwekeza nchini , kujenga miundombinu ya barabara, reli, umeme , viwanja vya ndege
na kuongeza uwekezaji katika utoaji wa huduma za jamii kama vile elimu, afya na
maji.
Aidha, ameeleza kuwa katika kufikia malengo hayo , Serikali
imefanya juhudi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusimamia vizuri ukusanyaji wa
mapato, kusimamia vizuri matumizi ya fedha za Serikali, kuongeza bajeti ya
maendeleo hadi kufikia asilimia kati ya 35 na 40 ya bajeti nzimat, kuongeza ufanisi
katika utendaji wa umma na kupambana na
rushwa pamoja na mambo mengine.
Pamoja na ukuaji mzuri wa uchumi, Dkt. Mpango alisema kuwa
Taifa bado linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ajira kwa
vijana, kiwango cha umasikini bado kiko juu, ukuaji mdogo wa Sekta ya kilimo ambayo imeajiri
takribani asilimia 70 ya watanzania unaosababishwa na ukosefu wa mbegu bora,
miundombinu ya umwagiliaji na soko la uhakika, na kupungua kwa mikopo ya benki
za biashara kwa sekta binafsi pamoja na mambo mengine.
Katika kusaidi juhudi za Serikali kupambana na changamoto
mbalimbali , Dk. Mpango aliiomba Benki ya Dunia kupitia kwa Dk. Felipe kuisadia
Serikali mkopo wa Dola za Kimarekani milioni 150 kwa ajili ya kuchochea ukuaji wa uchumi na
utoaji huduma ( Growth and Service Delivery) amabao uko katika hatua ya
maandalizi.
Mkurugenzi wa Uchumi Mpana, Biashara na Uwekezaji wa Benki
ya Dunia, Dkt. Felipe Jaramilo, kwa upande wake aliipongeza Serikali ya awamu
ya tano ya Dk. John Pombe Joseph
Magufuli kwa kazi nzuri inayofanya ya kusimamia uchumi mpana, kuongeza
makusanyo ya ndani ambayo yanasaidia upatikana fedha kwa ajili ya kugharamia uwekezaji
katika miradi mbalimbali ya maendeleo, kupambana na rushwa, kusimamia matumizi
ya fedha za umma, na kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi za umma.
Aidha, Dkt. Felipe aliishauri Serikali kuwekeza zaidi katika
rasilimali watu na miundombinu ili kulifanya Taifa kuweza kuhimili ushindani wa kimataifa dunia na kujenga uchumi unaokua na endelevu.
Vile vile aliieleza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita uwekezaji kutoka nje umekuwa
zaidi katika Sekta ya madini, hivyo alishauri Serikali kuweka mazingira mazuri
ya biashara ili kuwavutia wawekezaji kutoka nje kuwekeza katika sekta za
viwanda na utoaji huduma ili kuongeza wigo wa shughuli za kiuchumi na kuchochea
ukuaji wake.
Post a Comment
karibu kwa maoni