Serikali
ya Uingereza imeitaka Tanzania na Jumuiya ya Kimataifa kuiunga mkono
katika kupinga kitendo cha Urusi kutumia sumu aina ya novichok katika
jaribio la kumuua jasusi wa Kirusi, Sergei Skripal na binti yake, Yulia.
Tukio
hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita huko Salisbury, Uingereza na
kwa sasa Skripal na Yulia wana hali mbaya hospitali.
Akizungumza
na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, Balozi wa Uingereza
nchini, Sarah Cooke alisema nchi yake haitavumilia majaribio yoyote ya
mauaji ya watu wasio na hatia ndani ya ardhi yake.
Cooke
alisisitiza kwamba ni wazi Urusi ilihusika kwenye jaribio hilo na
walipewa nafasi ya kueleza kwa nini waliamua kutumia sumu hiyo ndani ya
Uingereza licha ya kwamba matumizi ya kemikali kama silaha ni kinyume
cha sheria za kimataifa. Hata hivyo, alisema mpaka sasa hawajatoa
maelezo kuhusu suala hilo.
“Baadaye
leo (jana) nitaonana na waziri wa mambo ya nje ili kumweleza kuhusu
jambo hili na kuomba ushirikiano wa Tanzania. Ninaamini Tanzania iko
pamoja nasi katika hili,” alisema balozi huyo.
Alipoulizwa
kuhusu msimamo wa Tanzania kuhusu suala hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya
Nje, Dk Susan Kolimba alisema hawezi kulizungumzia kwa sasa.
Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustine Mahiga hakupatikana kuzungumzia suala hilo .
Mpaka
sasa Uingereza inaungwa mkono na Marekani, Ufaransa, Ujerumani,
Austalia na Umoja wa Kujihami wa Nchi za Magharibi (Nato). Pia,
imeripoti suala hilo kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Pia imewatimua maofisa 23 wa intelijensia wa Urusi na imefuta ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Lavrov.
Vilevile,
Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May ametangaza kwamba hakuna waziri
yeyote au mtu kutoka familia ya kifalme atakayehudhuria Fainali za Kombe
la Dunia zinazotarajiwa kufanyika Juni huko Urusi.
Post a Comment
karibu kwa maoni