0
Image result for yanga vs stand unitedMABINGWA
watetezi, Yanga SC wameendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara baada ya kuibamiza Stand United mabao 3-1 katika
mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Ushindi
huo unaifanya ya kocha George Lwandamina anayesaidiwa na Mzambia
mwenzake, Noel Mwandila na wazalendo Nsajigwa Shadrack na Juma Pondamali
kufikisha pointi 46 baada ya kucheza mechi 21.


Yanga
sasa wanalingana kwa pointi na vinara wa muda mrefu msimu huu, Simba SC
ingawa mabingwa hao watetezi wamecheza mechi moja zaidi. 


Katika
mchezo wa leo, mabao ya Yanga SC yamefungwa na beki wa Stand United,
Ally Ally aliyejifunga, kiungo Ibrahim Ajib na mshambuliaji Mzambia,
Obrey Chirwa.


Alianza
beki Mzanzibari, Ally Ally kujifunga dakika ya saba katika harakati za
kuokoa mpira wa kiungo aliyepandishwa kutoka timu ya vijana, Yussuf
Mhilu.


Akafuatia
kiungo mshambuliaji mwenye mambo mengi uwanjani, Ibrahim Ajib Migomba
kufunga bao la pili dakika ya 12 akimalizia pasi ya Maka Edward na hadi
mapumziko, Yanga walikuwa wanaongoza kwa mabao 2-0.


Kipindi
cha pili, Stand United ya kocha Mrundi, Almasi Niyongabo anayesaidiwa
na wazalendo Athumani Bilal na Augustino Malindi kocha wa makipa,
ilibadilika na kuanza kuichezea Yanga.


Haikuwa
ajabu Stand United, maarufu kama ‘Chama la Wana’ mjini Shinyanga
walipofanikiwa bao dakika ya 84 lililofungwa na mshambuliaji wake, Tariq
Seif akiunganisha krosi ya Vitalis Mayanga.


Obrey
Chirwa akarejesha ushindi wa tofauti ya mabao mawili Yanga, kwa kufunga
bao la tatu dakika ya 85 akimlamba chenga kipa, Mohammed Makaka na
kufumua shuti nyavuni kufuatia pasi ya beki Said Juma ‘Makapu’
aliyepanda kusaidia mashambulizi. 


Baada
ya ushindi huo, Yanga SC inatarajiwa kuondoka Saa 10:00 Alfajiri kwenda
Botswana kwa ajili ya mchezo wa marudiano Raundi ya Kwanza Ligi ya
Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Township Rollers Jumamosi mjini
Gaborone.


Yanga
inahitaji ushindi wa ugenini wa 2-0 baada ya kufungwa 2-1 kwenye mchezo
wa kwanza wiki iliyiopita mjini Dar es Salaam ili kwenda hatua ya
makundi.      


Kikosi
cha Yanga leo kilikuwa; Youthe Rostand, Juma Abdul, Gadiel Michael,
Said Juma, Kelvin Yondani, Maka Edward, Yussuf Mhilu, Pius Buswita,
Obrey Chirwa, Raphael Daudi/Juma Mahadhi dk76 na Ibrahim Ajib/Emmanuel
Martin dk76.


Stand
United; Mohamed Makaka, Aron Lulambo, Miraji Maka/Makenzi Kapinga dk79,
Ally Ally, Erick Mulilo, Jisend Mathias/Ismail Gambo dk66, Bigirimana
Blaise, Abdul Swamad/Sixtus Sabilo dk79, Tariq Seifu, Ndikumana Seleman
na Vitalis Mayanga.


 

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top