Rais
wa Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB, Dkt. Akinumwi Adesina, amemaliza ziara
yake ya siku tatu nchini na kuahidi kuwa atahakikisha Tanzania inaendelea
kunufaika na misaada na mikopo yenye masharti nafuu kutoka Benki hiyo kwa ajili
ya ujenzi wa miundombinu ya kisasa katika Jiji la Dodoma na mradi wa kuzalisha
umeme wa Stieglers Gorge.
Akiwa
katika uwanja wa ndege Jijini Dodoma, Dkt. Adesina amemmwagia sifa Rais Dkt.
John Pombe Magufuli kwa namna anavyosimamia ukuaji wa uchumi uliofikia wastani
wa asilimia 7 kwa mwaka pamoja na kupambana na vitendo vya ufisadi, rushwa,
kuimarisha uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi, kupiga vita matumizi mabaya ya
rasilimali za umma ili kuwaondoa wananchi wake katika umasikini.
Dkt.
Adesina amesema kwa kutambua mchango huo pamoja na umahili wa Waziri wa Fedfha
na mipango Dkt. Philip Mpango, wa kusimamia uchumi na sera ya bajeti na fedha, benki
yake itaendelea kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha ili nchi iweze kupiga hatua
kubwa kupitia miundombinu mbalimbali inayotekelezwa kupitia benki yake na
washirika wengine wa maendeleo.
Miongoni
mwa miradi ambayo Benki hiyo imepanga kusaidia ni ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa utakaojengwa katika eneo la Msalato, nje kidogo ya Jiji la Dodoma
ambapo kwa kuanzia benki hiyo itatoa zaidi ya shilingi bilioni 200.
"Tumekuwa
na majadiliano ya kina na Mhe. Rais Dkt. John Magufuli kuhusu mradi wa
kuzalisha umeme wa Stieglers Gorge ambao utazalisha Kw 2100, Benki yetu
itaangalia namna ya kutoa fedha kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa mradi huo
mkubwa" alisema Dkt. Adesina.
Alisema
kuwa suala la mapinduzi ya viwanda haliwezi kufanikiwa bila kuwa na nishati ya
umeme ya uhakika na kwamba benki yake itawekeza dola za Marekani bilioni 1.5
kwa ajili ya sekta ya nishati na itaongeza kiasi kingine cha dola milioni 950
kwa ajili ya kazi hiyo.
"Mwaka
huu tutatoa fedha kwa ajili ya kuboresha nishati ya umeme katika ukanda wa
Kaskazini Magharibi mwa Tanzania na tuna mpango pia wa kuboresha Shirika la
Ugavi wa Umeme hapa nchini-TANESCO, ili liweze kuzalisha umeme wa uhakika na
wenye gharama nafuu kwa ajili ya kuendeleza mpango wa Serikali wa kuwa na
uchumi wa viwanda" aliongeza Dkt. Adesina
Kwa
upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameelezea
kufurahishwa na ujio wa Rais huyo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB, Dkt.
Akinumwi Adesina, na kwamba ujio huo umeleta neema kwa nchi baada ya benki hiyo
kuahidi kutoa shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kujenga Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Msalato pamoja na kuahidi kutoa fedha kwa ajili ya kujenga barabara za
mchepuko (mzunguko) Jijini Dodoma.
Dkt.
Mpango amewataka watanzania kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za
kuwaletea maendeleo na watembee kifua mbele kwa kuwa hivi sasa Tanzania
imeshika nafasi ya pili katika Bara la Afrika kwa ukuaji wa uchumi kwa kasi ikitanguliwa
na nchi ya Ethiopia, na Rais Adesina amelisemea vizuri jambo hilo.
Ushirikiano
wa Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB na Tanzania ulianza tangu mwaka 1971,
ambapo mpaka sasa benki hiyo imewekeza kiasi cha dola bilioni 3.6, sawa na zaidi
ya shilingi trilion 8, katika miradi mbalimbali ya kiuchumi ikiwemo umeme,
barabara, maji na usafi wa mazingira, uboreshaji rasilimali watu pamoja na
masuala ya utawala bora.
Post a Comment
karibu kwa maoni