Rais wa Benki ya Maendeleo
ya Afrika-AfDB, DKT. AKINUMWI ADESINA, ameanza
ziara ya kikazi ya siku tatu hapa nchini kwa mwaliko wa Rais Dkt. John Pombe
Magufuli na kuahidi kuwa benki yake itawekeza zaidi ya dola za Marekani bilioni
1 nukta 5 kwenye sekta mbalimbali katika kipindi cha miaka miwili ijayo,
Dkt. Adesina ameyasema
hayo alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam, na kupokelewa na mwenyeji
wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango.
"Tunajivunia uhusiano
wetu wa muda mrefu na Tanzania ambayo ni mnufaika anayeongoza miongoni mwa nchi
za kiafrika kupata ruzuku na mikopo yenye masharti nafuu kutoka benki yetu
ambapo tangu mwaka 1971, Benki imewekeza zaidi ya dola za Marekani bilioni
3.6" alisema Dkt. Adesina
Alisema kuwa miradi
inayoendelea hivi sasa nchini Tanzania kupitia ufadhili wa Benki yake imefikia
thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 2 ambapo uwekezaji mkubwa uko
katika sekta za nishati ya umeme, usafiri, miundombinu ya barabara, kilimo,
maji na usafi wa mazingira, kusaidia Bajeti Kuu ya Serikali pamoja na
uendelezaji wa rasilimali watu.
"Katika miundombinu
ya barabara peke yake, Benki yangu imewekeza zaidi ya dola za Marekani bilioni
1.1 na kwamba uwekezaji huo utasaidia kuboresha usafirishaji wa bidhaa na
abiria hivyo kuchochea ukuaji na uendelezaji wa uchumi wa viwanda" alisema
Dkt. Adesina.
Dkt. Adesina ameutaja
mradi mwingine mkubwa wa kusafirisha umeme wenye msogo wa kilovolti 400 wenye
njia yenye urefu wa kilometa 670 katika Ukanda wa Kusini na Kusini Magharibi
mwa Tanzania, unaohusisha pia ujenzi wa vituo vya kupozea umeme katika mikoa ya
Iringa, Dodoma, Singida na Shinyanga, wenye thamani ya dola milioni 220.
"Miradi hii pamoja na
ile wa umeme wa kutumia joto ardhi pamoja na maji inayotarajiwa kupatiwa fedha
na Benki hiyo, itasaidia sana mkakati wa Mhe. Rais Dkt. John Magufuli, ambaye
ammwagia sifa kwa utendaji kazi wake mahili, wa kujenga uchumi wa viwanda kwa
kuwa na umeme wa uhakika na wenye gharama nafuu" aliongeza Dkt. Adesina.
Alisema Tanzania imepiga
hatua katika viwango vya wananchi kupata huduma ya umeme ambapo awali ilikuwa
asilimia 18 lakini hivi sasa kiwango hicho kimepanda hadi kufikia asilimia 38
na kwamba lengo la benki hiyo ni kutaka kiwango hicho kifikie asilimia 82
katika miaka michache ijayo.
Alisema ili kufikia hatua
hiyo Benki yake ina mpango wa kuboresha Shirika la Ugavi wa Umeme
nchini-TANESCO ili liongeze uzalishaji wa umeme wenye gharama nafuu, kuongeza ufanisi
na kutengeneza faida ili kuchochea maendeleo ya viwanda.
Aidha, Rais huyo wa Benki
ya Maendeleo ya Afrika AfDB, ameeleza kuwa benki yake inasiadia kuendeleza
kilimo nchini kupitia Mpango wa Kukuza Kilimo katika Ukanda Kusini mwa Tanzania-SAGCOT,
kwa kukuza masoko na uongezaji thamani ya mazao ya wakulima yanayozalishwa
kupitia mradi huo.
Akizungumzia miradi ya
kikanda, Dkt. Adesina alisema kuwa benki yake imewekeza katika miradi ya
nishati ya umeme na miundombinu ya barabara ili kuunganisha Tanzania na nchi
jirani za Burundi na Kenya ili kurahisisha biashara na kuboresha upatikanaji wa
nishati ya umeme katika nchi hizo.
Kwa upande wake, Waziri wa
Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameeleza kuwa Benki ya Maendeleo ya
Afrika ni mshirika mkubwa wa Maendeleo wa Tanzania kutokana na uwekezaji mkubwa
uliofanywa katika nyanja mbalimbali.
Alisema kuwa AfDB, licha
ya kusaidia kwa kiasi kikubwa kufadhili miradi ya ujenzi wa barabara, nishati
na mingine mingi na mfuko mkuu wa Serikali, mwaja jana ilitoa pia mkopo nafuu
wa dola za Marekani milioni 50 kwa ajili ya kukuza mtaji wa Benki ya Maendeleo
ya Kilimo nchini-TADB, zinazotumika kukopesha wakulima.
Dkt. Mpango amesema kuwa
Rais huyo akiwa hapa nchini atatembelea mradi wa kituo cha kupooza umeme cha
Zuzu kilichoko mkoani Dodoma na ataungana na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe
Magufuli kuzindua barabara ya Dodoma-Babati hadi Arusha, iliyofadhiliwa na
Benki hiyo na washirika wake.
Post a Comment
karibu kwa maoni