Serikali imesema kuwa haitasitisha
mkataba na Mwekezaji wa Kampuni ya Chai Maruku, iliyoko mkoani Kagera, kwa
sababu mgogoro wa malipo uliopo baina ya kampuni hiyo na wakulima pamoja na wafanyakazi
wake unaelekea kutatuliwa.
Hayo yameelezwa leo Bungeni mjini
Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb),
alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Bukoba Vijijini Mhe. Jason
Rweikiza (CCM), aliyetaka kujua sababu za Serikali kutovunja mkataba na mwekezaji
huyo na kurejesha umiliki kwa Serikali au kwa mwekezaji mwingine atakayejali
maslahi ya wakulima na wafanyakazi.
Katika swali lake la msingi, Mhe. Rweikiza alisema kuwa tangu Kampuni hiyo ibinafsishwe
kwa mwekezaji, kumekuwa na malalamiko ya wakulima kutolipwa fedha za mauzo ya chai kwa wakati na
wafanyakazi kutolipwa mishahara na
stahiki zao ipasavyo.
Dkt. Kijaji alisema kuwa, katika
kutatua mgogoro huo Serikali kupitia ofisi ya Msajili wa Hazina imekuwa ikifuatilia
kwa karibu mwenendo wa utendaji na uendeshaji wa Kampuni hiyo kwa kufanya vikao
kwa nyakati tofauti kwa kushirikiana na ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya
Viwanda, Biashara na Uwekezaji, ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ofisi ya
Mkuu wa Mkoa Kagera, Bodi ya Chai na Wakala wa Maendeleo ya Wakulima wadogo wa
Chai (TASHTIDA).
Alisema kuwa katika vikao hivyo haki
ya kila upande ilizingatiwa ikiwemo suala la haki za wafanyakazi pamoja na
madai ya wakulima, ambapo mpaka sasa mwekezaji amekubali kulipa madai ya
wakulima kiasi cha Sh. milioni 12 huku wakiendelea kujadili namna ya kutatua suala
la madai ya wafanyakazi.
Dkt. Kijaji aliahidi kuwa Serikali
itaendelea kufuatilia kwa karibu suala hilo ili kuhakikisha haki za wakulima na
wafanyakazi hazipotei.
Imetolewa
na:
Benny
Mwaipaja
Mkuu
wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara
ya Fedha na Mipango
4/4/2018
Post a Comment
karibu kwa maoni