Mwenyekiti
Mtendaji wa IPP Dk Reginald Mengi ameingia ubia na Mwekezaji kutoka
India kujenga kiwanda cha dawa kitakachogharimu dola za kimarekani
milioni 55 sawa na shilingi bilioni 55 za Tanzania.
Ujenzi
wa kiwanda hicho kipya kiitwacho M- pharmaceutical Ltd, katika eneo
la Kerege, wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani umewekewa jiwe la msingi na
Waziri wa Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy
Mwalimu mwishoni mwa wiki.
Akizungumza
baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda hicho Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu
alimpongeza Dr Mengi kwa kutekeleza kwa vitendo agizo la Rais John
Magufuli alilolitoa wakati wa uzinduzi wa hospitali mpya kisasa ya
Taaluma na Tiba Muhimbili Mlonganzila.
Novemba
mwaka jana akifungua Hospitali hiyo katika hotuba yake Rais John
Magufuli aliwataka wafanyabiashara nchini kuanzisha viwanda vya dawa kwa
kuwa fedha nyingi zinatumika kuagiza dawa kutoka nje.
Dk
Mengi ambaye pia ni Rais wa sekta binafsi alikuwepo katika uzinduzi huo
na kusema kwamba yeye na wenzake watalitafakari rasmi suala hilo.
Waziri
Ummy Mwalimu pia amemhimiza Dr Mengi na mbia mwenzake kuharakisha
ujenzi wake na kumhakikishia kuwa bidhaa zitakazozalishwa zitapata soko
kubwa hapa nchini na nchi za ukanda huu, na kunufaika na upendeleo
maalum wa bidhaa zinazozalishwa nchini.
Akizungumza
katika hafla hiyo Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Dr Reginald Mengi amesema
katika awamu ya kwanza kiwanda hicho kitazalisha chupa milioni 30 kwa
mwaka za aina mbalimbali za maji ya dripu zinazotumiwa wakati wa
matibabu ya dharura nyakati za ajali, upasuaji, homa kali, na magonjwa
ya mlipuko, zinazokidhi vigezo vya kimataifa.
Amesema
kipaumbele cha ajira kitatolewa kwa wananchi wa Bagamoyo, na kusisitiza
kuwa umuhimu wa Watanzania kujiamini katika kujiletea maendeleo.
Mapema
Waziri wa Viwanda na Uwekezaji Dk Charles Mwijage na Mkuu wa mkoa wa
Pwani Mhandisi Evarist Ndikiro amewataka viongozi wasiwakwamishe
wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika maeneo yao.
Aidha
walisema kwamba serikali itashughulikia changamoto mbalimbali ikiwemo
upatikanaji wa maji, umeme wa uhakika na gesi asilia katika eneo hilo.
Alisema kwamba taifa linajenga uchumi wa viwanda na ni kazi ya serikali kuwezesha mazingira rafiki kwa ajili ya uwekezaji.
Uwekaji
jiwe la msingi ulishuhudiwa na wananchi wa Kerege, Balozi wa Ufaransa
Frederic Clavier, balozi wa China Wang Ke, Mbunge wa Bagamoyo Dr Shukuru
Kawambwa, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani Ramadhan Maneno na viongozi
mbalimbali mbalimbali wa serikali na CCM wa mkoa na wilaya ya Bagamoyo.
Post a Comment
karibu kwa maoni