Matukio ya utekaji na kupotea kwa watu yameibua mvutano baina ya wabunge, bungeni leo.
Mvutano
huo ulianza wakati mbunge wa Tabora Kaskazini (CCM), Almas Maige
akichangia bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya mwaka 2018/19 ya
Sh945.5 bilioni.
Katika mchango wake, Maige amegusia suala la matukio ya watu wasiojulikana akisema;
“Watu
wasiojulikana hawa wanaosemwa na wenzetu wa upinzani na huenda watu
wasiojulikana wanasema wanafanya kazi upande wa upinzani tu hapana. Mimi
nina orodha ya wana CCM waliofanyiwa na watu wasiojulikana.”
Kauli
hiyo haikupita hivi hivi, kwani mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita
Waitara alisimama kumpa taarifa Maige akisema idadi ya watu waliotendewa
uhalifu na watu wasiojulikana ni wengi, “Kuna utekaji, uonevu katika
nchi hii.”
Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga akamuuliza Maige, “Unapokea taarifa hiyo ya mheshimiwa Waitara.”
Kabla
hajajibu, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba akasimama na
kusema jeshi la polisi halijateka watu; “Mheshimiwa Maige anaongelea
watu wasiojulikana.”
Hoja
haikuishia hapo, Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia naye
akasimama na kusema, “Suala la uhalifu, halilinganishwi kwa vyama vya
siasa, sisi sote ni Watanzania na jeshi la polisi linalinda usalama wa
raia wote.”
Hapo ndipo Maige akapewa fursa na Mwenyekiti Giga kuendelea kuchangia akisema;
“Mimi siongelei uhalifu, naongelea watu kufanya matukio na hawakamatwi. Mimi nasema watu wanaofanya matukio wakamatwe.”
Bado mvutano uliendelea kwani, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Kunti Yusuph akasimama kumpa taarifa Maige kwa kusema;
“Suala
la kusema matukio yaliyofanyika upande wa upinzani na CCM hayafanani,
inadhihirisha kwamba Chama Cha Mapinduzi na Serikali yake imebariki
mfumo na matukio haya ili waje waseme Chadema ni wachache na CCM ni
wengi. Asante amedhihirisha.”
Akihitimisha
mchango wake kwa eneo hilo, Maige amesema, “Mimi nashangaa upande ule
(wa upinzani) wanakurupuka, mimi naongelea ombi langu kwa Serikali ili
kuweza kuwakamata watu wasojulikana.”
Post a Comment
karibu kwa maoni