0
KIJANA wa Kitanzania, Shujaa Suleiman Shujaa ameibuka kidedea na kitita cha sh. milioni 15 katika mashindano ya 19 ya Afrika ya kuhifadhi Quran kwenye kundi la washiriki wa juzuu 30.

Shujaa mwenye miaka 23 ambaye ni mkazi wa Morogoro, amejishindia pia laptop, kiwanja chenye hati eneo la Kigamboni kilichotolewa na kampuni ya Property International ya jijini Dar es Salaam pamoja na dola za Marekani 500 kutoka kwa Bw. Ahmed Seif “Magari” aliyetoa dola 500 kwa washindi wote watano.

Akizungumza na maelfu ya waumini na Watanzania waliofurika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana  mchana (Jumapili, Mei 27, 2018), Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waendelee kuilinda amani iliyopo nchini kwani ikipotea hakuna atakayeweza kufanya ibada.

“Mtakubaliana nami kuwa amani ya nchi yetu, ndiyo inatufanya tutembee vifua mbele dhidi ya wenzetu, ni neema kubwa ambayo kila muumini anapaswa kuilinda kwani ikipotea hata mkusanyiko wetu huu wa leo si rahisi kufanyika mahali kama hapa,” alisema.

“Leo hii tuko hapa uwanjani kwa sababu tuna amani, kama Serikali isingekuwa inashirikisha Watanzania wote kulinda amani, basi tusingeweza kukutanika hapa. Kuna nchi 18 ziko hapa, na watu wake wamekuja hapa uwanjani kwa kuwa wana uhakika na amani tuliyonayo sisi Watanzania,” alisema.

Alisema katika nchi ambazo amani imetoweka, watu wanalazimika kufanya shughuli za ibada majumbani au kwa kujificha. 
“Wenzetu hao, hawapati fursa adhimu kama hii ya kujumuika pamoja na majirani, ndugu, jamaa na marafiki kusikiliza na kufurahia kisomo cha Quran au kufanya shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii,” aliongeza.

Aliwataka Watanzania waendelee kubeza na kupuuza kauli za walio wachache ambao kwao kuzungumzia amani ni kujipendekeza kwa Serikali. “Watu hao wamesahau kwamba tofauti katika Uislamu hazikuanza leo, lakini tofauti hizo hazikuwa sababu ya wema waliotangulia kuacha kuheshimiana na kushirikiana,” alisisitiza.

Mshindi wa pili kwenye kundi hilo la juzuu 30 ni Ahmed Noor wa Sudan ambaye ameshinda sh. 12,564,750 pamoja na laptop akifuatiwa na Muzamil Awadh Mohamed wa Sudan alijishindia sh. milion 7.5 pamoja na laptop zilizotolewa na kampuni ya Camara Education.

Mshindi wa nne ni Abdulally A. Mohammed wa Kenya aliyepata zawadi ya sh. 5,711,000 na wa tano ni Ibrahim Maazur kutoka Niger, aliyepata sh. 3,426,000. Washindi hao wote watano walipewa zawadi ya kwenda hijja na Waziri wa Mambo ya Dini wa Saudi Arabia, Dk. Saleh Ally Sheikh.

Washiriki wengine kwenye kundi la juzuu 30 walitoka nchi za Rwanda, Burundi, Msumbiji Djibouti, Kenya, Ethiopia, Congo DRC, Nigeria, Ghana na Afrika Kusini.

Washiriki wengine waliopewa zawadi ni wale walioweza kuhifadhi Juzuu tatu (washindi watatu), Juzuu tano (washindi watatu); Juzuu 10 (washindi watatu) na Juzuu 20 (washindi watatu).

Viongozi wengine waliohudhuria mashindano hayo ni Makamu wa Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Dk. Mohammed Gharib Billal, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania kutoka Saudi Arabia, Comoro, Oman, Uturuki, Kenya, Msumbiji na Nigeria, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally na Rais wa taasisi ya Al-Hikma, Sheikh Sharif Abdilkadir Al-Ahdal.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemtaka Sheikh Nurdin Mohammed Ahmad (maarufu kama Sheikh Kishki) akaonane na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. William Lukuvi ili atoe maamuzi ya kiwanja chao kilichopo eneo la Matumbi ambacho mwaka jana aliagiza kifuatiliwe taratibu zake na kisha wapatiwe.

“Kuhusiana na suala la kiwanja mlichosema, mamlaka ya awali ni Manispaa ya Temeke na ilishakamilisha taratibu zote za kisheria, ikapeleka kwa Afisa Ardhi wa Mkoa kuona kama limepita kwenye vikao vyote ndipo wanaenda wizarani kupata kibali. Hakuna sababu ya wizara kuikatalia manispaa huku eneo lenyewe likiwa kwenye ramani kuu ya manispaa yenyewe, nenda mumuone Waziri mwenye dhamana, awape ardhi,” alisema.

Waziri Mkuu amefikia hatua hiyo baada ya kupewa taarifa akiwa jukwaani kwamba taasisi ya Al-Hikma iliwasiliana na Manispaa ya Temeke, hadi mkoani wakapewa barua zinaonyesha eneo liko sawa lakini walipofika wizarani wamekwamishwa na Afisa mmoja aliyemtaja kwa jina moja la Mama Mpetula.

Juni 11, mwaka jana katika mashindanio ya 18, taasisi ya Al-Hikma waliomba wapatiwe kiwanja na.118 kwenye kitalu E kilichoshikamana na kiwanja na. 117 chenye shule yao ya Al-Hikma Girls iliyoko Temeke ili waweze kujenga zahanati.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top