Waziri wa Fedha na
Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango, amewataka Watumishi wa Wizara hiyo kuongeza ukusanyaji
wa mapato na kusimamia nidhamu ya matumizi ya Fedha za Umma ili kuijengea Serikali uwezo wa kuwahudumia
wananchi na kuifanya nchi iwe na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Dkt. Mpango
ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi
wa Wizara hiyo uliowakutanisha wajumbe zaidi ya 190 kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Amesema kuwa Wizara
ya Fedha na Mipango inajukumu la kuhakikisha inatekeleza
usemi wa “Wizara ya Fedha na Mipango
ndiyo Moyo wa Serikali” kwa kutumia Baraza la Wafanyakazi katika kushauriana na
kuchangia mawazo yatakayosaidia katika
kutekeleza majukumu ya Wizara kama yalivyopangwa na kusukuma kasi ya maendeleo
ya uchumi wa Taifa.
“Watumishi wote wa
Wizara mnaowajibu wa kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kutumia utaalamu mlionao
na kutekeleza majukumu kwa kuzingatia nidhamu, maadili, sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa Umma ili kuongeza
tija” alieleza Dkt. Mpango.
Akizungumzia suala
la maadili Dkt. Mpango amesema kila mtumishi wa Wizara hiyo anapaswa kutunza
siri na nyaraka za Serikali kwa kuzingatia kuwa taarifa zinazopatikana kutokana
na majukumu haziachwi ovyo na hatimaye kuangukia mikononi mwa watu wasiohusika.
“Watumishi wote mnapaswa
kutotumia nyaraka au taarifa za ofisi za umma kwa masuala ya kisiasa kwani huo
ni uvunjaji wa taratibu za utumishi wa Umma”, alisisitiza Waziri Mpango.
Amesema kila
mtumishi anao wajibu wa kufanya kazi kwa bidii na kushirikiana kila mmoja
katika nafasi yake ili hatimaye Wizara ya Fedha iweze kufikia malengo iliyojiwekea
kwa mwaka ujao wa fedha 2018/2019 na kuchangia ipasavyo katika utekezaji wa
Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.
Dkt. Mpango,
amewaagiza watendaji wa Wizara hiyo kuhakikisha kuwa vikao vya Baraza la
Wafanyakazi vinafanyika kama vilivyopangwa kwa kuwa ni sehemu nzuri ya
wafanyakazi kueleza changamoto zao na kutoa mawazo namna ya kuboresha utendaji
kazi wa Wizara.
Kwa upande wake
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Doto James, amemhakikishia Waziri Mpango kuwa
watatekeleza maelekezo yote aliyoyatoa kwa ukamilifu ili kuongeza tija.
Akitoa maoni yake, Mhakiki mali za Serikali kutoka Mkoa wa Dar es
Salaam Bw. Ismail Ugaga ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Baraza hilo amesema kuwa
umefika wakati ambao Serikali inapaswa kuchukua hatua kali kwa wale wote
wanaotoa siri za Serikali ili kukomesha tatizo hilo miongoni mwa watumishi wa
umma.
Lengo kuu la Baraza la Wafanyakazi sehemu za kazi
ni kuongeza tija, ufanisi na ushirikishwaji wa wafanyakazi katika uongozi wa
pamoja mahali pa kazi kama linavyoagiza Agizo la Rais Na. 1 la mwaka 1970
likisomwa pamoja na miongozo mingine inayoyekeleza agizo hilo.
Post a Comment
karibu kwa maoni