0
RAIS Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) amewasili nchini kwa ziara rasmi ya kiserikali ya siku tatu na kupokelewa na mwenyeji wake, Rais John Magufuli.
Pamoja na Rais Magufuli, viongozi wengine waliompokea Rais Kabila jana alasiri ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa serikali, mabalozi na wananchi.
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, Rais Kabila alipokea heshima ya kupigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa ajili yake na baadaye kushuhudia burudani ya vikundi vya ngoma.
Leo Rais Kabila atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Rais Magufuli, ataweka jiwe la msingi la jengo la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na baadaye kushiriki dhifa ya kitaifa, iliyoandaliwa na mwenyeji wake, Rais Magufuli.
Rais Kabila aliwahi kusoma na kuishi nchini Tanzania. Lugha rasmi za DRC ni Kifaransa, Kilingala, Kikongo, Kiswahili na Kiluba.
Nchi jirani na DRC ni Kongo Brazaville, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan Kusini, Uganda, Rwanda, Burundi, Tanzania, Zambia na Angola.
Nchi hiyo ilipata Uhuru wake kutoka kwa Wabelgiji Juni 30, 1960.
Mwaka 1938 nchi hiyo ilikuwa na watu milioni 10, na mwaka 2015 idadi ya watu ilifikia milioni 81.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top