0
KATIKA gazeti la habari leo la jana, Mwinjilisti Jacob Foda wa kanisa la Waadventista Wasabato alikaririwa akisema ni jambo la kusikitisha sana kuona binadamu anatoa hukumu kwa mwenzake bila ya kumsikiliza.
Alisema hayo akizungumzia tukio la mauaji ya watafiti wawili na dereva katika kijiji cha Iringa Mvumi wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.
Mwinjilisti huyo ni sehemu ya kielelezo cha watu wenye ustaarabu, wanaofuata maadili na wenye kuheshimu uhai ambao wamekuwa hawaelewi kwa nini binadamu anaweza kutoa agizo la kuuawa kwa binadamu mwingine pamoja na kwamba amejieleza yeye ni nani na yupo hapo kwa sababu gani.
Aidha, maneno ya mwinjilisti huyo ni kielelezo cha ‘uungu’ wa binadamu katika sura sahihi ya Mungu mwenye upendo na anayejali maisha.
Pamoja na mwinjilisti huyo kutuonesha nini maana ya upendo na ufuataji wa ubinadamu, watunza sheria nao wamesema wazi kuwa kitendo hicho cha mauaji hayo hakikubaliki kwa namna yoyote ile na hata kwa sababu yoyote ile.
Kiukweli hapakuwapo na haja ya wananchi hawa kuwaua watu wale, kwani tayari walijisalimisha na walitaka wapelekwe kituo cha polisi kama walikuwa na shaka nao, lakini wananchi hao walihakikisha kwa jeuri waliyopewa na wakubwa wao wa imani wanatekeleza azma yao.
Huwezi kuacha kuamini kwamba hiyo ni jeuri ya kutoka kwa wakubwa kwa kuwa watu hawakutaka hata kutii hata risasi zilizopigwa na polisi walipofanya juhudi za kuwaokoa watafiti hao.
Tunaamini kwamba mauaji hayo yasingelikuwepo kama kusingelitokea watu wanaohimiza wenzao kufanya uhalifu kwa kuchukua hatua mikononi na hapa ndipo tuna kila sababu ya kulitaka jeshi la polisi kukamata na kuwafungulia mashtaka wanaohusika wote.
Na hii tunaona lazima ianze kwa mchungaji wa kanisa la Christian Family ambaye kwa makusudi akiwa na dhamira potofu kabisa, aliwatangazia watu wakafanye kosa la mauaji kwa kauli zake. Tulitarajia watu wa Mungu hawa kuwa na subira na roho za watu kwa kuwashawishi watu wao kutenda mema na kufuata sheria, lakini si jinsi alivyopiga unyende uliosababisha mauaji ya kutisha.
Iwe watu hawa wamekurupuka, au wamefanya wakiwa wanajua wanafanya nini, tunalishauri Jeshi la Polisi kuwapambanua watu hawa, hata kama wamekimbilia porini kuwakamata ili wakaonje sheria; ili pamoja na wao kujutia kila mmoja atakayefikiria kurudia kitendo hicho aone ‘moto’ wa sheria unavyounguza.
Pamoja na kumuomba Mungu awalaze pema peponi waja wake, Nicas Magazine aliyekuwa dereva pamoja na watafiti wawili, Teddy Lumanga na Jafari Mafuru, tunawataka wananchi kutambua kwamba hakuna sifa katika kutoa uhai wa mtu na wanaofanya kitendo hicho sheria itaona fahari wakikamatwa na kufikishwa kwake, hasa inapoonekana dhahiri kwamba kitendo hicho wamekifanya kwa makusudi kwa lengo lenye hila ovu dhidi ya ubinadamu.
Tunasema hata kama watakimbia mwaka mzima, watu hawa lazima wasakwe na wapelekwe mbele ya sheria kujibu hoja za mauaji, tena ya kukusudia huku wakiondoa nguvu kazi kubwa yenye kuwezesha maendeleo kwa kuwapa wananchi taarifa sahihi baada ya kufanya utafiti wa kina kuhusu namna ya kusonga mbele katika shughuli zao.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top