0
Licha ya serikali kusisistiza wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kupata chakula cha mchana Shuleni baadhi ya shule zimeshindwa kufanya hivyo kwa maelezo kuwa elimu ni Bure.
Shule nyingine hata kwenye vikao vinavyoitishwa kwa ajili ya kuweka utaratibu wa wanafunzi kupata chakula,mwitikio kwa wazazi umekuwa ni mdogo.
Akizungumza na kituo hiki ofisini kwake mkuu wa shule ya Sekondari Sigino katika Halmashauri ya mji wa Babati Mkoani Manyara Bi Leonardina Binamungu na msaidizi wake Paulo Niima wameeleza kuwa changamoto kubwa inayokwamisha jitihada za chakula cha mchana shuleni hapo ni ukosefu wa maji.
Kutokana na hali hiyo inawalazimu kuwaruhusu wanafunzi saa nane za mchana hivyo kukosa masomo ya jioni pamoja na michezo na kupelekea ufaulu kuwa mdogo.
''Katika miaka ya nyuma shuleni hapa wanafunzi walikuwa wakipatiwa chakula cha mchana ila tangu serikali iseme hakuna wazazi kuchangishwa,wazazi wamerudi nyuma".
"Mimi naona kuwa walipotoa sera hii kwamba wanafunzi wasichangishwe  wangetembelea na kuangalia  mazingira,sisi hapa tunakabiliwa na tatizo la maji'. aliendelea kusema mwalimu huyo.
Binamungu amesema kuwa ruzuku inayotolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza sera ya elimu Bure katika shule yake imekuwa ni kidogo kutokana na uchache wa wanafunzi.
"Shule hii ni ndogo inapata wanafunzi wachache,hii pesa tunayoletewa ya elimu bure ni kubwa kulingana na idadi ya wanafunzi,sasa shule hii ina wanafunzi kidogo na pesa inayoleta ni kidogo.Kifungu cha utawala tunapata shilingi elfu themanini na tano 85,000,kati ya hizo 60000 elfu tunalipa mlinzi,matuimzi ya maji kwa siku katika shule hii ni pipa tatu kwa shilingi elfu 15,000".
Mkuu huyo ameiomba serikali ya Halmashauri ya mji wa Babati na wizara husika kutatua changamoto zilizopo haswa hilo la maji ili shule hiyo iweze kuendelea mbele.
Shule hiyo ina nyumba mbili za walimu huku walimu wakiwa  19 ambapo katia ya hao wanaoishi kwenye nyumba za walimu ni watano pekee kutokana na ukosefu huo wa maji.
"Mimi nafikiri ufumbuzi wa changamoto hizi ni serikali kuleta maji ya uhakika katika shule hii".Alisema Binamungu
Katika halmashauri ya mji wa Babati shule ya Sekondari Sigino pekee ndio inayokabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa Maji na umeme.
Aidha ameongeza kwa kusema kwamba mpaka kufikia tarehe 18 Januari 2017 shule ilikuwa na wanafunzi 145,kidato cha kwanza [56]wavulana [23]wasichana [33],kidato cha pili [42] wavulana [19] wasichana [23],Kidato cha tatu [24] wavulana [9],wasichana [18],kidato cha nne [22] wavulana [10], wasichana [12].
Nao wanafunzi wakizungumzia adha wanayokutana nayo kutokana na ukosefu wa huduma ya chakula cha mchana na maji,wamesema inawafanya kufanya vibaya katika masomo yao kutokana na kukosa kwa masomo ya jioni kwani inawalazimu kutoka shuleni mapema ili kuwahi majumbani kupata chakula.
Kwa upande wa watoto wa kike wanasema wapo katika hatari ya kupata magonjwa ya kuambukiza kutokana na kukosekana kwa maji katika vyoo.
"Kuna muda inabidi tuache vipindi tukatafute maji na ni umbali mrefu sana zaidi ya kilomita 5"walisema baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne.
Wanafunzi hao wameiomba serikali itoe msaada katika shule hiyo ili wapate elimu bora na kufanya michezo katika shule hiyo.
Akizungumzia hilo katika Baraza la madiwani katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2017\2018 mkuu wa wilaya ya Babati Raymond Mushi alisema wanaendelea kufuatilia shule ambazo hazitoi chakula cha mchana kwa wanafunzi na kuwahamasisha wazazi kuchangia huduma hiyo.
"Chakula kwa wanafunzi ni lazima kila shule na haihusiani na elimu bure,wazazi wanatakiwa wachangie"alisema Mushi.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top