0


Kamanda wa Polisi Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya, ACP Mihayo Msikhela amedai wamejipanga kufanya msako dhidi ya wasanii wanatumia mihadarati hadharani.

Kamanda wa Kitengo cha Kupambana na Kudhibiti Madawa ya Kulevya, ACP Mihayo Msikhela
Akiongea na gazeti la Mtanzania, Kamishna huyo alisema wasanii ambao ndio kioo cha jamii, sasa wamekuwa wa kwanza katika kusambaza ujumbe wa matumizi hayo.
“Mimi binafsi simfahamu Chid Benz kama ni mtu maarufu aliyekuwa akifahamika kwa kiasi hicho, lakini baada ya kumuona kwenye mitandao ya kijamii ndipo nikaanza kumfuatilia,” alisema Kamishna Msikhela.
Alisema endapo wakipata taarifa ya kwamba wanatumia hadharani na kuwakamata, basi watachukuliwa hatua kama wahalifu wengine.
“Hawa wasanii tunawasaka nao watuhumiwe kama wahalifu wengine na wakichukuliwa hatua itakuwa fundisho kubwa kwa vijana ambao walikuwa na nia ya kujiingiza katika mtandao huo,’’ alisema.
Alisema ni vema kwa vijana wasiwafuate watu maarufu ambao kwa namna moja ama nyingine wanaushawishi mkubwa kiasi katika matumizi ya dawa hizo.
Kamishna Msikhela alisema wimbi kubwa la vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 30 ndilo ambalo linajiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya jambo ambalo ni hatari kwa Taifa.
“Vijana hawa ndio ambao wangekuwa tegemeo, vijana wa umri huo ndio ambao wangekuja kuwa viongozi wa baadaye, yaani kwa umri huo ndiyo wanaandaliwa kuwa madereva, mawaziri, wakulima, lakini leo wanakuwa mateja, ni jambo la hatari sana,’’ alisema.
Kamishna Msikhela alisema Jeshi la Polisi kwa sasa liko katika mkakati maalumu wa kuhakikisha elimu katika jamii inatolewa ili wananchi waweze kuelimika.
Alisema ulimaji wa bangi mashambani ni mkubwa kuliko mirungi, lakini aliongeza kuwa kama mateja mitaani wanapungua basi hata uingizaji wa dawa hizo kwa sasa nao umepungua.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top