Benny Mwaipaja-WFM, Dodoma
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amezitaka
Kampuni kubwa na za kati kuchangamkia fursa ya uwepo wa Sekta ya Soko la
Mipaji, kwa kujiorodhesha katika soko la hisa la Dar es salaam ili kushiriki
moja kwa moja katika umiliki wa uchumi wa nchi.
Dkt. Mpango ametoa rai hiyo Bungeni Mjini Dodoma, wakati
akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Jimbo la Magomeni, Mhe. Jamal Kassim
Ali, aliyetaka kujua mchango wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA)
na Soko la Hisa la Dar es saam (DSE), kwa wafanyabiashara wazawa.
Alifafanua kuwa kampuni kadhaa, ikiwemo Kampuni ya Bia
Tanzania (TBL), TOL Gases, Kiwanda cha Sigara (TCC), Kiwanda cha Saruji Tanga,
Wakala wa Huduma za Mizigo kwenye viwanja vya ndege-Swissport na Benki ya NMB,
ni baadhi ya kampuni zinazouza hisa zake katika Soko la Hisa la Dar es salaam.
Dkt. Mpango alisema kuwa kampuni hizo zimechangia kukuza uchumi
wa nchi ikiwemo ajira, kutoa gawiwo kwa Serikali na wanahisa, lakini pia ni
miongoni mwa walipa kodi wakubwa.
“Kwa mfano kwa mwaka
2015 NMB, ilitoa gawiwo Serikalini kiasi cha shilingi bilioni 16.5 na TCC shilingi
billion 1.4 kwa hisa zinazomilikiwa na Serikali huku mapato yatokanayo na kodi
pamoja na gawiwo, hutumiwa katika kutoa huduma mbalimbali ambazo jamii
ikijumuisha wafanyabiashara wadogo hunufaika nazo”alisema Dkt. Mpango
“Vilevile, Serikali imekuwa ikitumia masoko ya mitaji kama
chanzo cha upatikanaji wa fedha za bajeti (Treasury Bonds), Miradi inayotekelezwa
na fedha hizi, pamoja na mambo mengine, imekuwa ikitoa ajira na fursa za
kibiashara kwa wafanyabiashara wazawa; wadogo na wa kati” aliongeza Dkt. Mpango
Dkt. Mpango, alibainisha kuwa Serikali inatambua mchango
mkubwa wa kampuni ndogo ndogo katika kukuza uchumi wa nchi ndio maana mwaka
2013 Soko la Hisa la Dar es Salaam lilianzisha dirisha linaloziwezesha kampuni
ndogo na za kati za wazawa zisizokidhi vigezo vya kujiunga na soko hilo kupitia
dirisha kuu, kutumia Soko la Hisa katika kupata mitaji kutoka kwa umma wa
watanzania.
Dkt. Mpango alibainisha kuwa watanzania wengi wananufaika na
uwepo wa soko la hisa, na kushiriki moja kwa moja katika umiliki wa uchumi wa nchi
huku akizitaja baadhi ya kampuni zilizonufaika na utaratibu huo wa dirisha dogo
la hisa kuwa ni Benki ya Mwalimu
Commercial Bank, Swala Oil and Gas Tanzania, Maendeleo Bank PLC, Yetu
Microfinance na Mkombozi Commercial Bank, ambazo zina jumla ya mitaji isiyopungua
shilingi bilioni 120
Post a Comment
karibu kwa maoni