0
Benny Mwaipaja-WFM, Kyela
​​​​​​​​
Displaying IMG_6544.JPGKATIBU Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa Serikali inathamini mchango wa sekta ya biashara katika kukuza uchumi na maendeleo ya nchi hivyo itaendelea kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji biashara na uwekezaji.
Prof. Mkenda amesema hayo wilayani Kyela Mkoani Mbeya, wakati ujumbe wa Serikali ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban, ulipotembelea mpaka wa Tanzania na Malawi-Kasumulu, ili kujionea utendaji kazi wa Idara ya Forodha na Uhamiaji katika mpaka huo wa Kasumulu/Songwe.
Amesema kuwa Serikali inapohimiza ulipaji na kusimamia ulipaji kodi haina maana kwamba inawachukia wafanyabiashara, bali inatambua umuhimu wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa na kutoa wito kwa idara za Serikali zilizoko Mipakani kuboresha mazingira ya utoaji huduma ili kurahisisha biashara.
“Tunatakiwa kuondoa vikwazo vya ufanyaji biashara ikiwemo ucheleweshaji wa mizigo inayovushwa katika mipaka yetu kwa kuwa hatua hiyo itaongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam na kuzivutia nchi nyingi zaidi kutumia Bandari hiyo” Aliongeza Profesa Mkenda
Amewaonya watendaji wa Serikali walioko katika mipaka yote ya nchi, kuacha kufanyakazi kwa mazoea na kusisitiza kuwa wale wote watakaoshindwa keendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano ni afadhali wapishe kwa hiari yao.
Kwa Upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban, amesema kuwa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifawa miaka Mitano, unahitaji zaidi ya Shilingi Trilioni 107 na kwamba upatikanaji wa fedha hizo utahitaji mazingira bora ya kukuza uchumi wa nchi ikiwemo mazingira mazuri ya ufanyaji biashara mipakani
“Serikali itazifanyiakazi changamoto mlizozisema kama vile upungufu wa wafanyakazi, vitendeakazi na nyumba za watumishi, lakini wito wangu kwenu muendelee kufanyakazi kwa pamoja, mshirikiane kwa kuongeza nguvu ili kuongeza mapato ya Serikali” alisisitiza Bi. Amina Khmis Shaaban
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi, Balozi Hassan Simba Yahya, amelitaka jeshi la polisi hususan kikosi cha usalama barabarani kupunguza urasimu wakati wa kutekeleza majukumu yao wanapokutana na magari yaendayo masafa marefu nje ya mipaka ya Tanzania, wasiyacheleweshe njiani bila sababu za msingi.
Kwa upande mwingine, Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Bw. Qandiyay Akonaay, ameeleza kuwa TRA imeanzisha mfumo wa kufuatilia mwenendo wa mizigo inayosafirishwa kutoka Bandari ya Dar es Salaam, kwenda nchi jirani, hatua ambayo imeboresha kwa kiasi kikubwa ucheleweshaji wa mizigo na kwamba hatua hiyo pia imeongeza mapato ya kodi ya Serikali

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top