0
Watu wanne wamefariki na saba kujeruhiwa baada ya kufukiwa na kifusi walipokuwa wanachimba dhahabu katika mgodi usio rasmi kijiji cha Itumbi Kata ya Matundasi Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo mkuu wa Wilaya ya Chunya Rehema Madusa amesema waliofariki ni pamoja na Simon Majaliwa(25)mkazi wa kijiji cha Itumbi, Mazoea Mahona(25)mkazi wa Tabora,Benny Bahati(23)mkazi wa Mapogolo Chunya na James Alinanuswe(26)mkazi wa Tukuyu Rungwe.
Madusa amesema kuwa waliojeruhiwa ni Andrew Paul(26)mkazi wa Itumbi ,Marco Frederick(22)mkazi wa Itumbi,Isack James(30)mkaziwa Itumbi na Hamisi Mwalyosi (25)mkazi wa Mapogolo.
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Chunya amesema kuwa watu watatu walimbia baada ya tukio hilo ili kukwepa mkono wa sheria. Miili yote imetambuliwa na ndugu ambapo wamekabidhiwa kwa ajili ya taratibu za mazishi na majeruhi wamelazwa katika hospitali ya Wilaya ya Chunya wakipatiwa matibabu.Hata hivyo Madusa amesema kuwa watu hao walivamia mgodi huo asubuhi februari 20 mwaka huu ambapo mmiliki wake hajafahamika na kuanza kuchimba dhahabu bila kuchukua tahadhari hasa katika kipindi hiki cha mvua.
Baada ya udongo kuporomoka juhudi za uokoaji zilianza na watu saba walinusurika ambapo watatu walikimbizwa hospitali ya Wilaya ya Chunya na watatu walitokomea kusikojulikana. Mkuu wa Wilaya ametoa wito kwa wananchi kuacha kuendesha shughuli za uchimbaji bila kibali na kuchukua tahadhari hasa katika kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha mkoaani Mbeya.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top