
Hakimu
Mkazi, Desderi Kamugisha, amejitoa kuendelea kusikiliza moja ya kesi za
uchochezi zinazomkabili Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema
(Chadema).
Katika kesi hizo, Lema anadaiwa kutoa matamshi yenye chuki na kuibua nia ovu kwa jamii.
Hakimu
Kamugisha amejitoa katika kesi ya jinai namba 441/2016 ambayo Lema
anadaiwa kutoa matamshi hayo Oktoba 23, mwaka jana wakati wa mkutano wa
hadhara viwanja vya Shule ya Sekondari Baraa.
“Kiburi
cha Rais kisipojirekebisha, Rais akiendelea kujiona yeye ni Mungu,
mwaka 2020 haitafika Mungu atakuwa ameshamchukua maisha yake.
“Rais
ana kiburi, Rais kila mahali watu wanaonewa, wafanyakazi wa Serikali
hawana amani, wafanyabiashara hawana amani, watu wananyanyaswa,” Lema alinukuliwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Martenus Marandu.
Hakimu
huyo sasa ataendelea kusikiliza kesi nyingine ya jinai namba 440/2016
ambayo pia inamhusu Lema anayedaiwa kutoa maneno ya uchochezi yenye
kuleta tabaka miongoni mwa jamii Oktoba 22, mwaka jana maeneo ya Kambi
ya Fisi, Kata ya Ngarenaro wakati wa mkutano wa hadhara.
Miongoni mwa maneno ambayo Lema anayodaiwa kuyatoa ni: “Rais
Magufuli akiendelea na tabia ya kudhalilisha demokrasia na uongozi wa
upinzani, iko siku taifa litaingia kwenye umwagaji wa damu.
“Rais
yeyote ambaye haheshimu mipaka ya sheria, mipaka ya katiba, ataingiza
taifa katika majanga na umwagaji damu, watu watajaa vifua, wakiamua
kulipuka polisi hawa wala jeshi halitaweza kudhibiti uhalifu
utakaojitokeza.”
Jana
kesi hizo mbili zilipangwa kutajwa mbele ya Hakimu Kamugisha katika
Mahakama ya Wilaya ya Arumeru, lakini Wakili wa Serikali, Alice Mtenga,
alidai mahakamani hapo kuwa upelelezi umekamilika, hivyo wanaomba
kupangiwa tarehe ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali.
Lakini Hakimu Kamugisha alisema haoni busara kuendelea kusikiliza kesi zote wakati kuna mahakimu wengine.
“Nilikuwa
na kesi nne za mshtakiwa huyu huyu, sasa zimebaki mbili. Kwangu sioni
kama itakuwa busara kusikiliza kesi zote wakati kuna mahakimu wengine
wanaweza wakasikiliza, najiondoa kwenye kesi namba 441, nitaendelea na
kesi moja namba 440.
“Ukiangalia
nature ya kesi ni ile ile moja, mshtakiwa yule yule, kwa hiyo tutaenda
kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi ili apangiwe hakimu mwingine wa kusikiliza
kesi hiyo ili tarehe ya kusomwa maelezo ya awali itakayopangwa,
asikilize hakimu mwingine,” alisema.
Katika kesi hizo, Lema anawakilishwa na Wakili Sheck Mfinanga.
Hata hivyo, mshitakiwa huyo hakuweza kufika mahakamani hapo jana kwa madai kuwa hawakuwa na taarifa za kesi hizo kupangwa.
“Nilikuwa
nimesimama kwenye korido ya mahakama asubuhi nikamuona RCO, nikamuuliza
kuna nini akanijibu amekuja kwenye hizi kesi, ndipo nikaamua kuja
mahakamani ila Lema au wadhamini wake hawakufika,” alisema Mfinanga.
Lema alipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Kamugisha Novemba 8, mwaka jana, akikabiliwa na kesi hizo.
Novemba
11, mwaka huo huo, alishindwa kupata dhamana baada ya mawakili wa
Serikali kuwasilisha kwa njia ya mdomo kusudio la kukata rufaa Mahakama
Kuu Kanda ya Arusha, kupinga uamuzi wa dhamana uliotolewa na Mahakama ya
Hakimu Mkazi Arusha.
Lema
alikaa mahabusu ya Gereza Kuu la Kisongo kwa zaidi ya miezi minne
kutokana na kukosa dhamana kuanzia Novemba 11 mwaka jana kabla ya
kuachiwa kwa dhamana Machi 3, mwaka huu na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Post a Comment
karibu kwa maoni