Mfanyabiashara
wa Kariakoo, Casto Ngogo (35) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashitaka ya kukutwa na vifaa vya serikali
ambavyo ni suruali 5,000 sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ).
Ngogo
ambaye ni mkazi wa Tabata Segerea alifikishwa mahakamani hapo jana
mbele ya Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa na kusomewa mashitaka yake na
Wakili wa Serikali, Hamisi Saidi.
Akisoma
mashitaka, Wakili Saidi alidai Juni 15, mwaka huu maeneo ya bandari
kavu ya Galco iliyopo Chang’ombe wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, Ngogo
alikutwa na suruali 5,000 za JWTZ kwenye kontena namba PCIU 82851 (5) za
thamani ya Sh milioni 59 mali ya serikali bila kuwa na kibali.
Mshitakiwa
alikana mashitaka hayo upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa
shauri hilo haujakamilika na kwamba hawana pingamizi ya dhamana.
Hakimu
Nongwa alitaja masharti ya dhamana kwa mshitakiwa kuwa na fedha taslimu
Sh milioni 30 au hati ya mali isiyohamishika ya thamani hiyo pamoja na
wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh milioni 10 kila mmoja.
Ngogo alitimiza masharti hayo na kuachiwa huru ambapo kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 17 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.
Post a Comment
karibu kwa maoni