0
WAZIRI Mkuu, Kasim Majaliwa amepiga marufuku mtu yeyote kusafirisha mazao ya chakula kwenda nje ya nchi bila ya vibali.
Pia amesema Serikali inakusudia kutaifisha mahindi na vyombo vya usafiri vitakavyothibitika kusafirisha zao hilo kwenda nje ya nchi bila kibali maalumu. Kadhalika Majaliwa amepiga marufuku wafanyabiashara kusafirisha mahindi nje ya nchi bila ya kuyaongeza thamani na kuyasafirisha yakiwa ni unga. Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana wakati akitoa nasaha kwenye Baraza la Idd lililofanyika kitaifa kwenye msikiti wa Riadha, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro mara baada ya kuswali sala ya Idd.
“Kuanzia leo, ni marufuku kwa mtu yoyote kusafirisha mazao ya chakula kwenda nje ya nchi bila ya vibali. Serikali inahamasisha uwekezaji kwenye ujenzi wa viwanda nchini. Kama tutatoa vibali, ni lazima mtu alazimike kusaga nafaka ili kutoa ajira nchini. “Wote tunashuhudia baadhi ya mikoa ikikosa mvua za kutosha hivyo kuwa na upungufu wa chakula, ni marufuku kusafirisha mahindi kwenda nje ya nchi, kama ni lazima kupeleka nje basi uende unga na siyo mahindi,” alisema.
Alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira kupitia kamati yake ya ulinzi na usalama kujipanga vyema kudhibiti utoroshwaji wa chakula ikiwamo kuwachukulia hatua wale wote watakaokaidi maagizo halali ya serikali. Katika hatua nyingine Majaliwa alimtaka Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Hamisi Issah kuwachukulia hatua za kisheria baadhi ya maofisa wa polisi wanaosaidia uvushwaji wa chakula kwenda nje ya nchi kinyume cha utaratibu uliowekwa.
“Niliona kwenye televisheni malori zaidi ya 10 yaliyokamatwa Tarakea yakiwa na mahindi tayari kuvushwa mpaka... haiwezekani kukawa na mahitaji hayo, wakazi wa Tarakea hawazidi hata 4,000 iweje wapelekewe shehena ya Mahindi, hakikisheni hakuna mahindi yanayopelekwa nje,” alisema. Aidha, Waziri Mkuu alisema pamoja na kuwa na upungufu wa chakula katika baadhi ya maeneo bado taifa limepokea maombi ya chakula kutoka nchi za Congo, Somalia, Ethiopia na Sudan Kusini.
Aliongeza kwamba uhitaji huo usilete tamaa kwa wafanyabiasha kupeleka chakula katika nchi hizo na kutaka taratibu stahili zifuatwe kwani kinyume na hapo wahusika watachukuliwa hatua za kisheria. Hata hivyo, Majaliwa alitaja maeneo ya mipaka ya Tarakea, Holili, Mwanga, Horohoro, Siha, Namanga na Sirari imekuwa inapitisha kiasi kikubwa cha mazao ya chakula kwenda nje ya nchi jambo ambalo ni hatari.
“Hii ni kwa sababu chakula cha ndani hakitoshelezi mahitaji. Kwa sababu nchi zote za jirani hazina chakula cha kutosha. Tusipokuwa makini, tutabaki tunalia njaa,” alisisitiza. Alitumia fursa hiyo kuwasihi wafanyabiashara wa ndani, wachukue mahindi kutoka maeneo yenye mavuno mengi na kuyapeleka kwenye sehemu zenye mavuno kidogo. “Watanzania tushirikiane, kama ni biashara tutoe huku kwenye mavuno mengi na tuyapeleke Shinyanga na Geita ambako wanayahitaji au tukanunue Sumbawanga na kuyapeleka kwenye mikoa mingine yenye upungufu,” alisisitiza.
MAUAJI KIBITI Majaliwa alisema kuwa serikali kupitia vyombo vyake inafanya jitihada za makusudi kudhibiti kuendelea kwa mauaji ya raia, askari na viongozi wa kada mbalimbali wilayani Kibiti mkoani Pwani kwa kuhakikisha wanawakamata wanaohusika. “Yanayoendelea mkoani Pwani Serikali imejizatiti kuyakabili, maombi yangu ni raia wema kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola kwa kuwataja wale wote ambao wanahusika katika mauaji hayo... matukio haya hayahusiani na dini ya Kiislamu wala nyingine,” alisema.
DAWA ZA KULEVYA Majaliwa pia aliwataka viongozi wa dini waisadie Serikali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kupitia kwenye nyumba za ibada. “Naomba tuendelee kushirikiana kupambana na janga hili la dawa za kulevya kwa ustawi wa nchi yetu. Naamini viongozi wa dini mnayo nafasi kubwa katika mapambano haya, kwa kuwafunda vijana wetu kuishi katika maadili ya kidini na kutojiingiza kwenye janga hilo.”
Alisema Serikali kwa upande wake itaendeleza mapambano hayo bila ajizi wala mzaha. “Tunaomba wananchi wote watuunge mkono kwa kutoa taarifa sahihi za wanaojihusisha na uzalishaji, utengenezaji, usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya pindi tu wanapowabaini.”
PONGEZI KWA BAKWATA Waziri Mkuu pia alilipongeza Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kwa kuendelea kuwaunganisha Waislamu lakini pia kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kuleta maendeleo. “Naishukuru Bakwata kwa kuwa chombo imara cha kuwaunganisha Waislamu, kuhamasisha maendeleo kufuatilia mali za Waislamu na kutatua migogoro inayojitokeza maeneo tofauti, hata kuswali hapa Kilimanjaro ni kujenga umoja wa kitaifa,” alisema
. Katika hatua nyingine Waziri mkuu, ametaka Bakwata kutazama vyema mfumo wa kupata walimu wa dini, viongozi wa misikiti na vyuo vinavyofundisha wanafunzi elimu ya dini ili kuona kama inakidhi vigezo na kulijenga taifa imara.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top