0
Marehemu Philemon Ndesamburo
MAWAZIRI wakuu wastaafu na wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa na Frederick Sumaye pamoja na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe, leo wanatarajiwa kuongoza waombolezaji kuuaga mwili wa mwanasiasa mkongwe na Mbunge mstaafu wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo.
Viongozi wengine wanaotarajiwa kuwepo ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji, viongozi wa vyama vingine vya siasa, wabunge kutoka vyama mbalimbali vya siasa, wanasiasa, wafanyabiashara wakubwa wa ndani na nje ya nchi na wananchi wa kawaida. Katibu wa Chadema, Kanda ya Kaskazini, Amani Gulugwa alisema hayo wakati akielezea taratibu zilizopangwa za kuaga zitakazofanyika katika uwanja wa Majengo katika Manispaa ya Moshi na kwamba tayari viongozi wote wakuu wamefika mjini hapa huku mipango mingine ikiendelea kukamilishwa.
Alisema mwili utawasili uwanjani hapo leo saa 5:00 asubuhi, ambapo waombolezaji mbalimbali waliomfahamu Ndesamburo katika nyanja za kisiasa, biashara na utalii, michezo, dini, huduma za jamii na katika sekta ya habari watatoa heshima za mwisho na baada ya hapo mwili utarejeshwa nyumbani kwake Mtaa wa KDC, kata ya Kiboriloni, kwa ajili ya kusubiri maziko kesho, Juni 6 mwaka huu. ‘’Kwa sasa tunasubiri protokali za mkoa wa Kilimanjaro, ili kujua viongozi wa serikali kwa ngazi ya mkoa na taifa watakaokuja katika mazishi haya.
Tumeendelea kupokea salamu za rambirambi kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi,” alisema. Ndesamburo alifariki ghafla Mei 31 mwaka huu baada ya kupoteza nguvu za mwili na alifariki akiwa njiani kupelekwa katika hospitali ya Rufaa ya KCMC. Katika hatua nyingine, baadhi ya wakazi wa mjini Moshi wamesema leo watajitokeza kwa wingi kutoa heshima zao za mwisho kwa Ndesamburo aliyekuwa Mbunge wa Moshi Mjini kwa miaka mingi kwa sababu ya mchango mkubwa aliokuwa akiutoa katika jamii.
Walisema kwa nyakati tofauti kuwa Ndesamburo aliifanya Moshi kama sehemu ya familia yake kwa sababu hata baada ya kustaafu ubunge, aliendelea kutoa misaada na kuwa karibu na jamii. Mkazi wa Soweto, Juliana Mwasha alisema Ndesamburo ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Chadema, mkoani Kilimanjaro, alikuwa anatoa misaada mbalimbali kwa jamii bila kujali itikadi za vyama.
Mkazi wa Njoro, Elikunda John aliwaomba watu wajitokeze kutoa heshima za mwisho kwa Ndesamburo kwa sababu alikuwa anatoa misaada kwa wakazi wa Moshi hata nje na kueleza hata wakati mauti inamkuta alikuwa akisaini hundi ya rambirambi kwa wazazi waliofiwa na watoto kwenye ajali ya wanafunzi wa shule ya Lucky Vicent iliyotokea Mei 6, mwaka huu.
Chama cha waandishi wa habari mkoani Kilimanjaro (MECKI), pia kimeeleza jinsi Ndesamburo alivyokuwa akiwajali na kuwapa ushirikiano waandishi wa habari kwa sababu kila walipomhitaji alipatikana. Katibu wa chama hicho, Nakajumo James alisema, Ndesamburo alikuwa kiongozi wa makundi yote katika jamii pia alitoa ushirikiano na kuwathamini sana waandishi wa habari.
Alisema pamoja na ushirikiano aliokuwa akiwapa pia alikuwa akitoa msaada tangu chama hicho kilipoanzishwa mwaka 1999, na alitoa msaada wa kompyuta ambayo walikuwa wakiitumia, pia mwezi mmoja kabla ya kifo chake alitoa pikipiki ambayo kila mwaka watakapokuwa wanapata fedha watakuwa wanamkumbuka.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top