Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Pamoja na malalamiko na manung’uniko ya hali ngumu
ya maisha kwa watanzania wengi, Tanzania ndio yenye kiwango cha chini cha
mfumuko wa bei wa wastani wa asilimia 6.1 kwa mwezi Mei 2017 kwa nchi za Afrika
Mashariki.
Hayo yamebainishwa leo bungeni Mjini Dodoma na
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akiwasilisha Taarifa ya Hali ya
Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2017/18.
Mhe. Dkt. Mpango amesema mfumuko wa bei katika
nchi za Afrika Mashariki kwa mwaka 2016 uliendelea kuwa wa kiwango cha tarakimu
moja, ambapo Rwanda ilikuwa na asilimia 7.1, Uganda asilimia 5.4, Tanzania
asilimia 5.2, Kenya asilimia 6.3 na Burundi asilimia 5.6.
Alisema kufikia mwezi Aprili 2017, mfumuko wa bei
kwa nchi hizi ulipanda, ambapo kwa Burundi ulifikia asilimia 21.10, Rwanda
asilimia 13.0; Kenya asilimia 10.28; Uganda asilimia 6.4 na Tanzania asilimia
6.4.
“Hata hivyo, kwa upande wa Tanzania mfumuko wa bei
umeendelea kushuka mpaka asilimia 6.1 kwa mwei Mei 2017” amesema Dkt. Mpango
Mhe. Dkt Mpango amesema kwa miaka minne mfululizo,
wastani wa mfumuko wa bei kwa Tanzania umeendelea kupungua, ukibaki katika
kiwango cha tarakimu moja.
Amesema kwa mwaka 2016, mfumuko wa bei ulifikia
wastani wa asilimia 5.2 ikilinganishwa na asilimia 5.6 mwaka 2015. Kupungua kwa
wastani wa mfumuko wa bei nchini kulichangiwa kwa kiasi kikubwa na: mwenendo wa
kushuka kwa bei za mafuta ya petroli katika soko la dunia na nchini; kuimarika
kwa upatikanaji wa vyakula nchini na hivyo kuimarisha wastani wa bei; na kuwepo
kwa sera madhubuti za usimamizi wa bajeti na fedha.
Mhe. Dkt. Mpango amesema mfumuko wa bei
uliongezeka kidogo, ambapo ulifikia asilimia 6.4 mwezi Aprili 2017 lakini ukiwa
ndani ya maoteo ya wastani wa tarakimu moja (asilimia 5 – 8) kwa mwaka 2017.
Hali ya kuongezeka kwa mfumuko wa bei nchini
ilichangiwa na hofu iliyotokana na kuchelewa kwa msimu wa mvua katika maeneo
mengi nchini na hivyo kuwepo kwa taharuki ya kutokea upungufu wa chakula. Hata
hivyo, maeneo mengi yamepata mvua ya kutosha na hivyo bei ya chakula nchini inatarajiwa kupungua.
Mhe. Dkt. Mpango amesema kasi ya ukuaji wa uchumi
katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ilishuka kutoka wastani wa asilimia 6.5
mwaka 2015 hadi asilimia 5.3 mwaka 2016 ijapokuwa Jumuiya hii iliendelea
kuongoza kwa ukuaji miongoni mwa Jumuiya mbalimbali za Afrika.
Amesema kasi ndogo ya ukuaji wa uchumi katika
Jumuiya hii ilichangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo kushuka kwa bei za bidhaa
na kudorora kwa uchumi wa dunia. Maoteo ya mwenendo wa uchumi katika ukanda huu
yanaonesha utakua kwa wastani wa asilimia 5.7 mwaka 2017 na asilimia 6.0 mwaka
2018.
“Matarajio haya yanazingatia hatua zinazochukuliwa
na nchi za ukanda huu katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na uendeshaji
biashara kama vile kuwa na maeneo tengefu ya ujenzi wa viwanda (industrial
parks), hususan, vya nguo, bidhaa za ngozi, kilimo, madawa na vifaa tiba”
ameongeza Dkt. Dkt. Mpango
Amesema kwa nchi za Jumuiya
ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), kasi ya ukuaji wa uchumi ilishuka
kutoka wastani wa asilimia 1.9 mwaka 2015 hadi asilimia 1.1 mwaka 2016.
Mhe. Dkt. Mpango amesema kasi
ndogo ya ukuaji wa uchumi katika Jumuiya hii ilichangiwa na uhaba wa nishati ya
umeme pamoja na ukame uliochangiwa na mabadiliko ya hali ya hewa ya La Nina.
Amesema licha ya kasi ndogo
ya ukuaji, Jumuiya hii iliendelea kuwa ya tatu kwa ukuaji miongoni mwa Jumuiya
za barani Afrika na unatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 1.4 mwaka 2017.
Waziri wa Fedha amesema
mfumuko wa bei ulifikia asilimia 10.5 mwaka 2016 ikilinganishwa na asilimia 5.7
mwaka 2015, ukichangiwa na ukame na kuyumba kwa utekelezaji wa sera za mapato
na matumizi kwa baadhi ya nchi wanachama.
Post a Comment
karibu kwa maoni