Zikiwa zimebaki siku mbili kufika tarehe 15 zilizoongezwa na Serikali kwa wananchi kulipa kodi ya
majengo bila adhabu, baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wameiomba
Serikali iongeze muda mwingine zaidi ili watu wote waweze kulipa kodi hiyo bila
adhabu kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati wa zoezi hilo.
Wananchi hao wamemweleza Waziri wa
Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango alipofanya ziara za kushitukiza katika
Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA-Mtaa wa Kipata-eneo la Mnazi Mmoja na
Mbagala mkoani Dar es Salaam
Wamesema kuwa mwamko wa wananchi kulipa
kodi ni mkubwa hali iliyosababisha foleni kubwa kila mahali nchini kutokana na
uhaba wa watumishi wa TRA pamoja na vitendeakazi muhimu kama vile kompyuta na
mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFDs).
Waziri wa Fedha na Mipango Dokta Philip
Mpango amewataka Watanzania kuwa watulivu na kuendelea kulipa kodi hiyo huku
akiahidi kutatua changamoto ya uhaba wa watumishi pamoja na vitendeakazi ili
kuwaondolea adha wananchi waliojitokeza kwa moyo kulipa kodi mbalimbali ikiwemo
ya majengo.
Ameahidi pia kwamba Serikali
itayafanyiakazi maombi ya wananchi ya kutaka kuongezewa muda wa kulipa kodi
hiyo na kwamba watajulishwa wakati muafaka uamuzi wa Serikali kuhusu
suala hilo.
Dokta Philip Mpango amesema kuwa
Serikali inafarijika kwa kiasi kikubwa na namna wananchi walivyoitikia wito wa
Mheshimiwa Rais Dokta John Pombe Joseph Magufuli unao wataka wananchi walipe
kodi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Amebainisha kuwa watu wanapolipa kodi
wanaipa nguvu Serikali ya kuboresha huduma za jamii kwa wananchi ikiwemo elimu,
barabara, maji, afya na kuboresha huduma ya umeme hususan vijijini na kulifanya
Taifa kupunguza utegemezi wa misaada kutoka nje ya nchi.
Majuma mawili yaliyopita Serikali
iliongeza muda kwa wananchi kulipa kodi ya majengo bila adhabu kwa muda wa
majuma mawili hadi Julai 15 mwaka huu ambapo siku hizo zitaisha siku ya
Jumamosi huku idadi kubwa ya watu ikiwa bado wanahitaji kulipa kodi hiyo.
Post a Comment
karibu kwa maoni