0
MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Kanda ya Afrika Mashariki, Dkt. Nyamajeje Weggoro, amewataka wanafunzi 45 kutoka Tanzania, Kenya, Uganda na Ethiopia, wanaosoma katika Chuo Kikuu cha Nelson Mandela cha Sayansi na Teknolojia kilichoko mkoani Arusha, kusoma kwa bidii na maarifa ili waweze kuzisaidia nchi zao kuinua sekta ya viwanda kwa njia ya utafiti na ubunifu wa teknolojia mbalimbali

Dkt. Weggoro ametoa rai hiyo alipotembelea Chuoni hapo ili kuangalia utekelezaji wa programu ya miaka mitano ya kuboresha masuala ya rasilimali watu inayofadhiliwa na Benki yake kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 8.2

Alisema kuwa Benki yake imeamua kuwekeza fedha nyingi katika eneo la Sekta ya elimu ya juu katika nyanja ya ufundi ili kuwapata vijana wa kutosha watakaoziba pengo lililopo na kuweka misingi mizuri ya maendeleo ya baadae hasa katika matumizi ya teknolojia na sayansi.

 “Nimefurahi sana kuona wanafunzi wanasoma na wana ari kubwa na kwamba fedha tulizozitoa zinatumika vizuri, tunadhani hata baada ya mradi huu wa  miaka 5 kukamilika, Benki itaweza kusaidia zaidi ufadhili wa fedha na vifaa” Alisema Dkt. Weggoro.

Kaimu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela, Prof. Joram Buza, ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB kwa ufadhili huo, hatua iliyoongeza udahili wa wanafunzi katika chuo hicho.

“Mwaka wa masomo wa 2014/2015, Chuo kilidahili wanafunzi 7 pekee kutokana na changamoto wafadhili lakini baada ya ufadhili wa AfDB na Benki ya Dunia, wanafunzi wameongezeka hadi kufikia 135 jambo linalotia matumaini” alisema Pro. Buza.

Bi. Mwanaisha Mkangara na Bw. Alexander Mzura, wanaosomea shahada ya uzamivu katika masuala ya uhandisi na mifugo, kupitia ufadhili wa AfDB, wamesema kuwa masomo yao yatawaongezea ujuzi wa namna ya kufanya utafiti wa kihandisi na kuvumbua chanjo mbalimbali za mifugo.

AfDB inafadhili wanafunzi 45 ambapo 42 kati yao wanatoka Tanzania, huku Uganda, Kenya na Ethipia zikitoa mwanafunzi mmoja mmoja.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top