
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema jana kuwa tukio hilo la uporaji na unyang’anyi wa kutumia silaha lilitokea Julai 17, mwaka huu, ambako majambazi wapatao watano walivamia kiwanda hicho wakiwa na mapanga, mawe na nondo na kumpiga mlinzi wa kiwanda hicho na kitu kizito kichwani na kuzirai.
Kamanda Msangi alisema baada ya kumpiga mlinzi huyo, walimpora mlinzi huyo silaha aina ya shortgun aliyokuwa nayo na kuitumia kufanya uhalifu kiwandani hapo kwa kupora kiasi hicho cha fedha huku wakiwajeruhi wamiliki wa kiwanda hicho na kukimbia kusikojulikana.
Alisema baada ya tukio hilo kutokea, polisi walifanya ufuatiliaji wa kuwatafuta majambazi hayo na ndipo walipofanya ufuatiliaji na msako wa kuwatafuta sehemu mbalimbali za Mkoa wa Mwanza na maeneo jirani, ambapo wakati msako ukiendelea polisi walipokea taarifa za kiitelijensia kuwa majambazi hao wamekimbilia mkoani Singida.
“Ndipo askari wetu walikwenda mkoani Singida na kushirikiana na askari wa mkoa wa Singida walifanikiwa kuwakamata majambazi wawili na kurudi nao Mwanza”, alifafanua. Aliwataja majambazi hao waliokamatwa Julai 19 mwaka huu mkoani Singida kuwa ni Seif Waziri (37) na Kaini Mwakalinga (35) wote wakazi wa Dodoma, wakiwa na fedha Sh milioni mbili na Dola za Marekani 20,000 na silaha aina ya shortgun yenye namba za usajili 011765714 iliyosajiliwa na Jeshi la Polisi nchini na kupewa namba 00107210.
Alisema katika mahojiano ya awali na watu hao baada ya kufikishwa jijini Mwanza, walikiri kuhusika kwenye tukio la uvamizi wa kiwanda hicho cha kutengeneza mabondo cha kampuni hiyo ya Kichina. Alisema walikwenda kuwaonesha polisi sehemu walikokuwa wameficha silaha na kumtaja mwenzao mwingine, Emmanuel Mwakilili ambaye ni mkazi wa Dodoma na Dar es Salaam na ambaye pia anashikiliwa na jeshi hilo. Watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa.
Post a Comment
karibu kwa maoni