Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
SERIKALI ya China imeipatia Tanzania msaada wa Shilingi
bilioni 29.4 kwa ajili ya kusaidia sekta ya elimu ya ufundi stadi, utalii wa
kijiolojia na kukarabati wa Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Makubaliano ya msaada huo yametiwa saini Jijini Dar es
Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James, kwa niaba
ya Serikali, na Kaimu Balozi wa China hapa nchini, Mhe. Gou Haodong.
Bw. Doto James alisema kuwa kiasi cha Shilingi bilioni 22.4
cha msaada huo kitatumika kujenga Chuo cha Ufundi Stadi-VETA wilayani Ngara
mkoani Kagera, ambacho kitakapo kamilika kitadahili zaidi ya wanafunzi 400.
“Fedha hizo zitatumika kujenga vyumba 19 vya madarasa,
ujenzi wa karakana 9 za kutolea mafunzo ya elektroniki, ufundi bomba,
useremala, ufundi uashi na upakaji rangi” alisema Bw. James
Alieleza kuwa kiasi hicho pia kitatumika kujenga
majengo ya utawala, mabweni, nyumba za walimu na miundombinu mingine
itakayosaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwenye chuo
hicho.
“Tunaamini kwamba msaada huo utakuwa sehemu ya kusaidia
jitihada za Serikali za kujenga uwezo wa wataalamu wake watakaochangia kukuza
sekta ya uzalishaji na hatimaye kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira kwa
vijana nchini” alisema Bw. James
Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto
James alibainisha kuwa katika makubaliano ya msaada huo, Jamhuri ya watu wa
China, itatoa kiasi cha shilingi bilioni 6.7 kwa ajili ya kuukarabati Uwanja wa
Taifa wa Michezo wa Dar es Salaam.
“Katika makubaliano yetu ya msaada wa kuendeleza Uwanja wa
Taifa wenye uwezo wa kuingiza watu 60,000, China itatoa msaada wa kiufundi na
vifaa vya kisasa vya michezo na utaalamu katika usimamizi na ukarabati wa
uwanja” Alifafanua Bw. James
Bw. Doto James alisema kuwa kiasi kingine cha shilingi
milioni 300 kitatumika kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa
kuanzishwa kwa aina mpya ya utalii ujulikanao kama utalii wa kijiolojia
“Geopark Project” katika Hifadhi ya Taifa Ngorongoro, mkoani Arusha.
Alisema lengo la utafiti huo ni kuhakikisha kuwa Tanzania
inanufaika na maajabu mbalimbali ya kitalii yaliyopo nchini ambayo hayajatumika
kikamilifu kuvutia watalii watakaoongeza pato la Taifa
“Tanzania ina kila sababu ya kujifunza kutoka katika Hifadhi
ya Kimataifa ya Jiolojia ya Jiaozuo ya Yuntaishan ya China, iliyoanzishwa mwaka
2000 ambayo inaongeza asilimia 37.2 ya watalii kila mwaka na huchangia asilimia
12 ya pato la Taifa la nchi hiyo” aliongeza Bw. Doto James.
Aliishukuru China kwa ushirikiano wake wa dhati na Tanzania
tangu miaka ya 1960 na kwamba mpaka sasa nchi hiyo imeendelea kuipiga jeki
Serikali katika ujenzi wa miradi mbalimbali ukiwemo upanuzi wa Chuo cha Polisi
Moshi, Ujenzi wa Maktaba mpya katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na ujenzi wa
Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kwa upande wake Kaimu Balozi wa China hapa nchini, Mhe. Gou
Haodong, amesema kuwa nchi yake inatarajia kwamba ujenzi wa Chuo Cha Ufundi
VETA huko Ngara mkoani Kagera utaanza haraka kama ilivyopangwa.
Kuhusu masauala ya utalii wa kijiolojia katika Hifadhi ya
Taifa Ngorongoro, alisema Tanzania ina bahati ya kuwa na vivutio vingi vya
utalii lakini haijavutia idadi kubwa ya watalii kutoka China kuja kuvitembelea.
“Zaidi ya watalii milioni moja kutoka China wanatembelea
nchi mbalimbali dunia lakini kati ya hao, Tanzania inapokea watalii elfu 20 tu
kila mwaka kutoka China, lakini kwa kuanzisha mradi huu, watalii wengi kutoka
China watavutiwa kuja nchini kufurahia utalii wa miamba, mandhari nzuri, urithi
wa dunia, na kutembelea hifadhi za Taifa” aliongeza Mhe. Haodong
Akizungumzia masuala ya uchumi, Balozi huyo alisema kuwa
hivi sasa China imekuwa mwekezaji mkubwa zaidi nchini Tanzania kwa kuwekeza
kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.77 na kukuza ajira nchini.
Ameitaja baadhi ya miradi mikubwa iliyowekezwa kuwa ni
pamoja na mradi wa miundombinu ya mtandao (Tanzania ICT Broadband
backbone), Bomba la gesi la kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, mradi wa
kuboresha miundombinu ya Bandari, barabara na madaraja.
Hafla hiyo imehudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo, ambaye alisema kuwa msaada
wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi VETA mkoani Kagera kitaongeza watalaamu watakaosaidia
kuendeleza sekta ya viwanda nchini.
Post a Comment
karibu kwa maoni