0
#Anaandika Benny Mwaipaja, Kagera

Displaying IMG_1208.JPGNAIBU waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, ameziagiza Mamlaka na Taasisi zote za Umma kufanya ununuzi wa vifaa na mafuta kupitia Wakala wa Serikali wa ununuzi na ugavi (GPSA) kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge na kuwaonya wahusika wote watakaoendelea kukaidi maagizo hayo kwamba watachukuliwa hatua za kisheria.

Dkt. Kijaji ametoa maagizo hayo mkoani Kagera baada ya kutembelea na kukagua shughuli zinazofanywa na Wakala wa Ununuzi na Ugavi GPSA mkoani humo na kubaini kuwa taasii na idara nyingi za umma zinafanya manunuzi nje ya mfumo wa GPSA jambo ambalo amesema ni ukiukwaji mkubwa wa sheria.

Alisema kuwa lengo la Serikali la kuanzishwa kwa wakala huo pamoja na mambo mengine ilikuwa kudhibiti matumizi ya Serikali na kuonya kuwa Serikali haitakubali kuona sheria zinakiukwa kwa makusudi na kwa malengo yanayoonesha kuna nia isiyo njema katika matumizi ya fedha za umma.

“Hili si ombi ni maelekezo na ni agizo, taasisi zote zipate huduma kutoka kwa wakala wetu (GPSA) kwani Serikali ilikuwa na dhamira ya uwepo wa matumizi sahihi ya fedha za matumizi wanazopelekewa na ndiyo maana ukaanzishwa Wakala huu” Alisema Dkt. Kijaji

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawiro, akizungumza kwaniaba ya Mkuu wa mkoa wa Kagera, aliiagiza Wakala wa Ununuzi na Ugavi (GPSA) mkoani humo kumpelekea orodha ya taasisi ambazo hazitumii huduma za wakala huo ili aweze kuchukua hatua.

Alisema kuwa ni jambo lisilofaa kwa Taasisi za Umma kukiuka sheria na kwamba watatekeleza maelezo yaliyotolewa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango haraka ili kuokoa fedha za Serikali na kuweka uwajibikaji.

Awali, Kaimu Mkuu wa Wakala wa Ununuzi na Ugavi GPSA mkoa wa Kagera Bi. Dorothea Bugenyi alieleza kuwa katika kipindi cha miaka 3 iliyopita Wakala huo umeongeza makusanyo yatokanayo na mauzo ya vifaa na mafuta kutoka Shilingi bilioni 1.9 hadi kufikia Shilingi bilioni 2.34.

Alisema kuwa mapato hayo yangekuwa makubwa zaidi endapo taasisi zote za umma zingetii sheria na kufanya manunuzi yao ya vifaa na mafuta kutoka kwa Wakala huo na kuiomba Serikali kuusaidia Wakala huo kuziagiza taasisi zake za umma kutekeleza sheria hiyo kwa vitendo.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top