0
Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima RamadhaniTUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza majina 27 ya wagombea udiwani walioteuliwa na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kuwania nafasi hizo katika kata 10 zitakazofanya Uchaguzi Mdogo Februari 17, mwaka huu.
Uchaguzi huo unafanyika katika kata hizo kutokana na baadhi ya madiwani kujiuzulu nyadhifa zao na vifo. Katika uteuzi huo, wanaume waliojitokeza kugombea nafasi hizo ni 24 wakati wanawake ni watatu.
Kwa mujibu wa taarifa ya NEC, katika uteuzi huo, wagombea wa kata nne waliteuliwa Januari 20 na wagombea wengine wa kata sita waliteuliwa Januari 24, mwaka huu.
Iliwataja wagombea waliojitokeza kuwania udiwani katika Kata ya Buhangaza iliyoko Wilaya ya Muleba mkoani Kagera na vyama vyao ni Jenitha Tibihenda (CCM), Nelson Makoti (Chadema) na Grayson Aniceth (NCCR Mageuzi).
Katika Halmashauri ya Siha iliyoko mkoani Kilimanjaro ambako kuna kata tatu zitakazofanya Uchaguzi Mdogo, wagombea waliojitokeza katika Kata ya Gararagua ni Zakaria Lukumai (CCM) na Agness Lasway (Chadema); Kata ya Donyomuruak, wagombea ni Lwite Ndossi (CCM) na Daniel Mollel (Chadema) wakati katika Kata ya Kashashi ni Suzan Natai (CCM) na Immanuel Saro (Chadema).
Mkoani Mwanza ambako kuna kata mbili, wagombea katika Kata ya Kanbyelele iliyoko Halmashauri ya Misungwi ni Marco Yela (ACT Wazalendo), Daniel Makoye (CCM) na George Mhoja wa Chadema wakati Kata ya Isamilo wilayani Nyamagana wagombea ni Nyamasiriri Marwa (CCM), John Kisyeri (Chadema), Hashim Ramadhan (CUF), Georgina Kibendegele (DP) na Ramadhani Mtoro wa UDP.
Kwenye Kata ya Mitunguruni iliyoko Wilaya ya Singida wagombea ni Abdallah Mkoko (CCM), Manase Kijanga (Chadema) na Abdallah Kinga wa CUF. Wagombea Kata ya Madanga iliyoko Wilaya ya Pangani mkoani Tanga ni Mohamed Abdallah (ACT Wazalendo), Athuman Tunutu (CCM) na Swaibu Mwanyoka wa CUF.
Katika Mkoa wa Dodoma ambako pia kata mbili zitafanya uchaguzi, kwenye Kata ya Manzase wilayani Chamwino Jimbo la Mtera wagombea ni Amos Mloha (CCM), Alex Chalo (Chadema) na Ndahani Mazengo wa CHAUMMA, wakati Kata ya Kimagai iliyoko wilayani Mpwapwa, mgombea Noah Lemto ambaye amepita bila kupingwa.
Uchaguzi huo utaenda sambamba na uchaguzi wa wabunge katika majimbo mawili ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam na Siha mkoani Kilimanjaro. Katika Jimbo la Kinondoni, walioteuliwa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo kuwania ubunge ni wagombea 12 ambao ni Godfrey Maliza (TLP), Johnson Mwangosi (SAU) na Mwajuma Milambo kutoka UMD.
Wagombea wengine ni John Mboya (Demokrasia Makini), Maulid Mtulia (CCM), Mary Mpangala (DP), Salim Mwalimu (Chadema), Rajabu Salum (CUF), Mohamed Majaliwa (NRA), George Christian (CCK), Ally Omari Abdallah (ADA -Thadea) na Ashiri Kiwendu wa AFP.
Kuhusu uteuzi wa wagombea ubunge katika Jimbo la Siha, walioteuliwa ni wanne ambao ni Dk Godwin Mollel (CCM), Mdoe Yambazi (SAU), Tumsifuheri Mwanry (CUF) na Elvis Mosi wa Chadema. Kampeni katika kata 9 na majimbo hayo mawili zinaendelea kufanyika hadi Februari 16, mwaka huu.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top