Viongozi watano wa Chadema kati ya
saba waliokwenda Kituo Kikuu cha Polisi kuitikia wito wa kamanda wa
polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, wameachiwa kwa dhamana.
Walifika kituoni hapo leo Februari
20, 2018 saa 6: 10 mchana na kuachiwa saa 7:45 mchana.
Viongozi walioitwa na Mambosasa ni
mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vincent
Mashinji, naibu makatibu wakuu John Mnyika (bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar).
Pia wamo, mwenyekiti wa Baraza la
Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee; mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti, John
Heche na Esther Matiko ambaye ni mweka hazina wa Bawacha.
Waliofika leo kituoni hapo na
kuachiwa ni Bulaya, Mdee, Matiko, Heche na Mnyika.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake,
Mnyika amesema kupitia wakili wao, Peter Kibatala wamepewa dhamana na
kutakiwa kuripoti tena kituoni hapo, Februari 27, 2018.
Amedai kuwa fununu zilizopo ni
kwamba wanaweza kufunguliwa shataka la kuandamana bila kuwa na kibali.
"Tumefika hapa lakini
hatujahojiwa hivyo tumepewa dhamana na tutaripoti siku ya Jumanne wiki ijayo,”
amesema.
Wito wa viongozi hao polisi umekuja
siku siku nne tangu kutokea kwa kifo cha Akwilina Akwiline, mwanafunzi wa mwaka
wa kwanza wa Chuo cha Taifa cha Usfairishaji (NIT).
Akwilina aliuawa kwa kupigwa risasi
Februari 16, 2018 akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni, Kinondoni jijini
Dar es Salaam wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakienda
ofisi za mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni kudai viapo vya mawakala wao.
Post a Comment
karibu kwa maoni