0
Makamu wa Rais, Samia SuluhuWAKATI wanawake nchini leo wanaungana na wenzao duniani, kusherehekea Siku ya Wanawake duniani, Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kuwawezesha wanawake kwenye mambo saba makuu, katika kuimarisha usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake vijijini.
Makamu wa Rais, Samia Suluhu kupitia kaulimbiu ya ‘Kuelekea Uchumi wa Viwanda: Tuimarishe Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake Vijijini’, amewataka wanawake kutambua kuwa serikali imekuwa ikiwahudumia, kuwathamini, kuwawezesha na kuwasimamia vyema ili kuhakikisha usawa wa kijinsia unakuwepo katika jamii.
Alisema, “Mimi kama mwanamke na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nina kila sababu ya kuzungumza japo kwa kifupi jitihada mbalimbali zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na serikali katika kuimarisha usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake Vijijini.” Makamu wa Rais alibainisha mambo hayo saba kuwa ni: Kuwepo kwa Sera ya Kuendeleza Wanawake, Sheria za Ardhi za mwaka 1999 ambazo husimamia haki za wanawake katika kumiliki ardhi, lakini pia Sera ya Elimu Bure inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano, ambayo imetoa fursa kwa watoto wengi wa kike kuandikishwa shuleni.
Alisema jambo lingine ni kuwa kuboreshwa kwa huduma za kijamii, kama vile kujengwa zahanati na vituo vya afya na usambazaji wa maji, vimempunguzia mwanamke usumbufu na hivyo kumpa muda wa kutosha kufanya shughuli za maendeleo. Pia, alisema usambazaji umeme vijijini, kwa kiasi kikubwa umesaidia wanawake wengi, kujishughulisha na shughuli mbalimbali za kujiingizia kipato.
Lakini, pia uwezeshaji wa wanawake kwa kuwapatia asilimia 5 ya mapato ya halmashauri na asilimia 30 ya zabuni za halmashauri, kumewawezesha wengi kufanya biashara na hatimaye kuwa na uhakika wa kipato. Aliongeza, “Serikali kuendelea kuhimiza taasisi za kifedha kutoa mikopo yenye riba nafuu ili kuwawezesha wanawake wengi kunufaika na mikopo.
Pia kurasimisha vikoba pamoja na kuwashawishi wanawake wengi zaidi kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuweza kunufaika na mafao na mikopo itolewayo na taasisi hizo.” KIUCHUMI Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, kuhusu maadhimisho ya Siku ya Wanawake duniani, ilisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kuwezesha wanawake 772.075 kiuchumi, kwa kutoa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 13.7.
Kwamba mikopo hiyo, ilitolewa kwa wanawake hao waliojiunga katika vikundi vya kiuchumi wengi wao wakiwa wanawake wa vijijini. ELIMU Waziri Ummy alisema kuwa serikali hiyo, ilifanikiwa kutoa elimu ya msingi na sekondari hadi kidato cha nne bila malipo na kuwezesha kufikiwa kwa uwino 1:1 kwa wanafunzi wasichana na wavulana katika shule za ngazi husika. MAAMUZI Alisema kuwa serikali iliridhia Itifaki ya Maendeleo na Jinsia ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika. Alisisitiza ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi kwa asilimia 50.
Alieleza kuwa “Kutokana na utekelezaji wake Tanzania imefanikiwa kufikia asilimia 37 ya wanawake Bungeni, asilimia 41 wanawake majaji na asilimia 30 wanawake madiwani... kutokana na jitihada hizo wanawake wanaendelea kuaminika na kuchukua nafasi za juu za uongozi na maamuzi ikiwemo nafasi ya Makamu wa Rais na Naibu Uspika.” HAKI Alisema kuwa Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ya kisheria kwa wanawake ili kuwawezesha kupata haki zao za msingi, ikiwemo kuzifanyia marekebisho sheria mbalimbali, kutunga sheria zinazowezesha upatikanaji wa haki kwa wanawake na kutoa mafunzo na msaada wa kisheria kwa wanawake.
KWA NINI SIKU YA WANAWAKE? Akielezea Siku ya Wanawake duniani mwaka huu, Ummy alisema Tanzania kama zilivyo nchi nyingine za Umoja wa Mataifa, imekuwa ikiadhimisha Siku ya Wanawake Duniani Machi 8 kila mwaka. Kwa mara ya kwanza maadhimisho hayo yalifanyika nchini mwaka 1997 na kuanzia mwaka huohadi mwaka 2005, yalikuwa yakiadhimishwa Kitaifa kwa kila mwaka.
Alisema lengo la kuadhimisha siku hiyo ni kutathmini utekelezaji wa afua za kufikia usawa jinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi, kijamii, kisiasa katika kufikia maendeleo jumuishi. Maadhimisho hayo, pia yanatoa fursa ya kuelimisha jamii kuhusu jitihada mbalimbali zilizofanywa na jamii, serikali, asasi za kiraia, sekta binafsi na wadau wa maendeleo katika kumwinua mwanamke wa kitanzania.
MAFANIKIO KIMATAIFA Waziri Ummy alisema kutokana na jitihada hizo za serikali na wadau wengine, Jukwaa la Uchumi Duniani katika Taarifa yake ya mwaka huu kuhusu viashiria vya maendeleo jumuishi, imeiweka Tanzania katika nafasi ya kwanza Barani Afrika kwa kuwa na uchumi jumuishi. Taarifa hiyo kimsingi inaonesha namna ambavyo Tanzania inayapa kipaumbele na kuyashughulikia masuala ya usawa ikiwemo usawa wa jinsia.
Pia alisema kutokana na Mkutano wa Nne wa Dunia kuhusu Wanawake, uliofanyika Beijing China mwaka 1995, masuala ya jinsia na uwezeshaji wanawake yameendelea kupewa msukumo mkubwa zaidi. KAULIMBIU YA DUNIA Mwaka huu, kaulimbiu ya kimataifa inasema, “Changamoto na fursa za kufikia usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wanaoishi vijijini.”
Katika muktadha wa Tanzania, kaulimbiu ya mwaka huu ni “Kuelekea Uchumi wa Viwanda: Tuimarishe Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji Wanawake Vijijini.” WIZARA YA ELIMU Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia elimu msingi, Dk Avemaria Semakafu wakati akizungumza katika kongamano la Siku ya Wanawake, lililoandaliwa na serikali ya Uingereza jana, alisema kuwa serikali inakamilisha ukarabati wa shule za sekondari za ufundi ili kuwasaidia wanafunzi kujifunza masuala mbalimbali ya ubunifu kwa kutumia sayansi na teknolojia ya kisasa.
MWANAFUNZI, MTAALAMU Mwanafunzi mwenye ulemavu wa kusikia anayesoma shahada ya pili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Aneth Isaya anasema wakati dunia inasheherekea Siku ya Wanawake, wenye ulemavu wameachwa nyuma kwa kutengwa kuanzia ngazi ya elimu hadi kwenye ajira. Aneth ambaye pia ni Mwanzilishi wa Asasi ya Wanawake Wajasiriamali Viziwi Tanzania, alisema hayo jana kwenye mjadala wa siku ya wanawake uliofanyika katika Ukumbi wa Nkrumah, UDSM.
Akiwakilisha wanafunzi wenzake chuoni hapo, Aneth alisema mazingira ya elimu kwa wenye ulemavu ni magumu, lakini alihakikisha anapambana ili afaulu kwa kuomba uongozi wa chuo umsaidie kumtafutia mkalimani wakati anasoma shahada ya kwanza, ili aweze kutimiza ndoto yake katika elimu. Mkurugenzi wa Kitengo cha Jinsia UDSM, Dk Eugenia Kafanabo alisema matamasha kama hayo, lengo ni kukumbushana kujua umuhimu wa kina mama katika jamii yetu, hivyo viongozi waichukue ni nafasi ya kuboresha mazingira bila kuwepo kwa ubaguzi wa aina yoyote.
WANAHARAKATI Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Edda Sanga alisema kaulimbiu hii inawataka wanajamii kushirikiana kikamilifu, kubadilisha maisha ya wanawake kwa kuondokana na ukatili wa kijinsia ili kupanua wigo wa fursa za usawa kiuchumi kwa wanawake Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA), Tike Mwambipile alisema “Wanawake wa vijiji ndiyo wanashiriki kwa kiwango kikubwa katika maendeleo, ukiangalia kilimo ndiyo uti wa mgongo wa nchi yetu na walimaji wakubwa ni wanawake waliopo pembezoni hivyo ni muda wa wao kuangaliwa.”
WADAU WENGINE Leo wanawake watapata fursa, kukutana kwenye kongamano, lililoandaliwa na Mradi wa Kutambua Wanawake wenye Mafanikio Nchi kwa Kuwatunuku Tuzo (TWAA), unaolenga kuwatambua wanawake wenye mchango chanya katika maendeleo ya jamii watapewa tuzo. Mwanzilishi wa tuzo hizo kupitia TWAA, Irene Kiwia aliweka wazi kuwa watatoa tuzo.
Tuzo hizo zinazofanyika kila baada ya mwaka mmoja, zinatimiza mwaka wa sita. Zimewaongezea hamasa wanawake wengi nchini, huku wengine wakiongezewa uelewa wao katika masuala ya kumkwamua mwanamke. Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu alisema siku ya leo wanazindua mfuko maalumu wenye vifaa vya kujifungulia kwa akina mama. Lengo la hatua hiyo ni kuendelea kuboresha sekta ya afya kwa kuhakikisha dawa na vifaa vyote muhimu vinavyohitajika, vinapatikana kwa kutosheleza mahitaji.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top